WASHINGTON, MAREKANI
RAIS wa Marekani, Donald Trump, ametangaza ushuru wa asilimia tano kwa bidhaa zote zinazotoka nchini Mexico, ili kuishinikiza nchi hiyo kuchukua hatua kali zaidi kuwazuia wahamiaji haramu kuingia Marekani.
Ushuru huo utaanza kutozwa rasmi kuanzia Juni 10 mwaka huu na unaweza kupanda mpaka asilimia 25 hadi tatizo hilo la wahamiaji litakapokuwa limedhibitiwa.
Uamuzi huo wa Trump unaonesha kuwa, Serikali ya Marekani itachukua hatua mpya za kuongeza mbinyo kwa Mexico kama ilivyokuwa kwa China kuchukua hatua hata kama zitahatarisha vipaumbele vya sera nyingine kama za makubaliano ya biashara huru kati ya Marekani, Mexico na Canada, ambayo ni msingi wa ajenda ya Trump bungeni na yanayoweza kumnufaisha katika juhudi zake za kuchaguliwa tena.