MGOMBEA urais kutoka Chama cha Republican, Donald Trump amewasilisha sera yake mpya ya mageuzi ya uhamiaji huku akiapa kuwafungulia mashitaka wanawake wanaomtuhumu kuwadhalilisha.
Aidha alisema atapunguza kodi kwa tabaka la kati kwa asilimia 35 wakati wa siku zake 100 za kwanza madarakani, iwapo atashinda urais mwezi ujao.
Trump pia alitumia hotuba hiyo ya sera kuwaambia wasikilizaji wake: “Kila mwanamke aliyeongopa, kwa matukio ambayo hayakuwepo na waongo wote hawa watafikishwa mahakamani baada ya uchaguzi huu,” alisema.
Licha ya kitisho hicho, mwanamke mwingine alijitokeza baadaye siku hiyo akisema Trump alimnyanyasa kimapenzi miaka 10 iliyopita wakati wa mashindano ya golf huko Lake Tahoe, California.
Mwanamke huyo, ambaye ni mcheza filamu za ngono, Jessica Drake, alisema Trump alimvamia na kumbusu bila ruhusa yake na baadaye kuahidi kumpatia dola 10,000 iwapo angekubali kutumia jioni ya siku hiyo katika ndege yake binafsi.
Anadai kukataa ofa hiyo na kwamba amejitokeza ili kuungana na wanawake wengine waliojitokeza kumshutumu Trump kwa unyanyasaji dhidi ya wanawake.
Ikiwa zimebaki siku 17 kabla ya uchaguzi mkuu wa Novemba 8, Trump alitoa hotuba ya sera zake huko Gettysburg, Pennsylvania, karibu na eneo a vita ya wenyewe kwa wenyewe ambako Rais wa zamani Abraham Lincoln alitoa moja ya hotuba muhimu zaidi katika historia ya Marekani miaka 153 iliyopita.
Trump alisema atakomesha mmiminiko wa wahamiaji haramu nchini hapa na kwamba ataweka kifungo cha chini cha kuanzia miaka miwili kwa yeyote atakayeingia isivyo halali pamoja na kitaongezeka kwa kadiri ya makosa yanavyoongezeka kabla ya kuwatimua.