LUCIANA LUAMBANO (TUDARCO) Na LEONARD MANG’OHA
-DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), inatarajia kutumia zaidi ya Sh trilioni 1.3 kujenga miradi mitatu ya kukusanya, kuondoa na kusafisha majitaka katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Romanus Mwang’ingo, alisema ujenzi huo utahusisha mitambo ya kusafisha majitaka yatakayotumika kwa shughuli mbalimbali ikiwamo kupoozea mitambo viwandani.
Alisema mradi huo utaongeza kiwango cha kusafisha majitaka kutoka asilimia 10 za sasa hadi 30 ifikapo 2020.
Aidha, alisema mradi wa kwanza utajengwa katika eneo la Jangwani utakaokuwa ukikusanya majitaka kutoka Ubungo, Mwananyamala, Kinondoni katikati ya jiji, Ilala na Msasani.
“Mradi huu utakuwa na uwezo wa kusafisha mita za ujazo 200,000 kwa siku utakaokuwa na mabomba yenye urefu wa kilomita 376.
“Pia katika awamu hii ya kwanza bomba linalomwaga majitaka baharini litaacha kutumika, baadala yake majitaka hayo yatasafishwa katika mtambo huo ambao unajengwa kwa ushirikiano na Serikali za Tanzania na Korea Kusini kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya Korea na utagharimu Dola milioni 90 ambazo tayari zimepatikana,” alisema Mwang’ingo.
Aidha, tayari taratibu za manunuzi zinaendelea ili kumpata mshauri na mkandarasi ili kuanza kazi ya ujenzi mapema mwakani, ambapo mradi wa pili utahusisha ujenzi wa mtambo wa kusafisha majitaka eneo la Mbezi Beach na Kilongawima.
Alisema mtambo huo utakaokuwa na uwezo wa kusafisha mita za ujazo 16,000 kwa siku, utajumuisha mfumo wenye urefu wa kilomita 97 utakaoanzia Mbezi Beach, Kilongawima, Kawe, Tegeta na maeneo jirani.