KOKU DAVID-DAR ES SALAAM
Mamlaka ya ya Mapato Tanzania (TRA), imesema jamii ina jukumu la kuhakikisha kila mwenye mapato anatakiwa kulipa kodi ili kuweza kuimarisha miundombinu na mifumo mingine itakayowezesha kuendesha maisha ya kila siku.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Agosti 1, baada ya mkutano ya Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Msafiri Mbibo, amesema TRA itaendelea kuboresha mazingira mazuri ya wafanyabiashara ili waweze kufanya biashara zao vizuri na kulipa kodi kwa hiyari.
Alisema sambamba na hilo pia wataendelea kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake ili kuwawezesha kukokotoa kodi vizuri pasipo kumuonea mtu lakini pia serikali iweze kupata kodi yake stahiki.
“Tutaimarisha mifumo ya kuwezesha TRA na wafanyabiashara kuwasiliana vizuri lakini pia wafanyabiashara nao wanatakiwa kuungana katika makundi ili kuweza kuongea lugha moja na serikali,” amesema.
Amesema TRA imeweka utaratibu wa kutana na wafanyabira wote nchi nzima kwa lengo la kubadilishana uzoefu ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto wanazokutana nazo ili kuweza kuzitafutia utatuzi.