29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yatoa mwongozo mashine za EFD zinapoharibika

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM              |            


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiashara kutoa taarifa ya maandishi iwapo Mashine yake ya kutolea Risiti za Kielektroniki (EFD) itaharibika.

Taarifa hiyo inatakiwa kutolewa ndani ya saa 24 katika ofisi ambako mashine hiyo ilinunuliwa ikiwa ni pamoja na kupeleka kopi ya barua hiyo katika ofisi ya TRA pamoja na kitabu cha risiti za mkono ili waweze kupata kibali cha kutoa risiti za mkono hadi mashine yake itakapokaa sawa.

Aidha mfanyabiashara huyo atatakiwa kupeleka kopi hiyo ya barua katika ofisi za TRA  ambako analipia kodi zake.

Kwa mujibu wa TRA, tatizo la kuharibika haribika mashine hizo za EFD limeshatatuliwa na kwamba wafanyabiashara wanatakiwa kuacha kutoa sababu za kuharibika kwake.

TRA ambayo jukumu lake ni kukusanya mapato ya serikali yanayotokana na kodi ikiwa ni pamoja na yasiyotokana na kodi imekuwa ikiwasisitiza wafanyabiashara kutumia mashine za EFD ili kuweza kukusanya mapato stahiki kwa mujibu wa sheria.

Kamishna wa Kodi za Ndani, Elijah Mwandumbya anasema kuwa tatizo la mashine za EFD limeshatatuliwa na kwamba mashine itakayoharibika mfanyabiashara atatakiwa kuandika barua yenye kutoa taarifa za kuharibika kwa mashine hiyo ndani ya saa 24 sehemu ambako mashine hiyo ilinunuliwa.

Anasema pia atatakiwa kupeleka kopi ya barua hiyo pamoja na kitabu cha risiti za mkono katika ofisi za TRA ambako analipia kodi zake ili kiweze kuwekewa muhuri wa mamlaka hiyo kama kibali cha kukitumia kwaajili ya kutolea risiti pindi anapomaliza kutoa huduma kwa mteja wake hadi hapo mashine hiyo itakapokaa sawa.

Anaongeza kuwa, baada ya kupona kwa mashine hiyo mfanyabiashara atatakiwa kuingiza taarifa zote kwenye mashine ya EFD za mauzo yote aliyoyafanya pindi akitumia risiti za mkono ili mapato ya serikali yaweze kufika kihalali.

Mwandumbya anasema kuchelewa kutoa taarifa ni kosa kisheria kutokana na kuwa kutokutoa risiti ni kuiibia serikali mapato yake na kwamba faini itatolewa dhidi ya mfanyabiashara huyo atakayebainika kutokutoa taarifa za kuharibika kwa mashine yake.

Anasema kuwa mfanyabiashara atakayebainika hajatoa taarifa za kuharibika kwa mashine yake faini yake ni milioni 3 kama ni kosa lake la kwanza lakini kama makosa yakijirudia atatozwa hadi  milioni 4.5 pamoja na kifungo ili kutoa fundisho kwa wengine ambao sio wazalendo kwa nchi yao.

Anasema kwa upande wa muuzaji wa mashine hizo anatakiwa kuwa ameitengeneza mashine hiyo ndani ya saa 48 tangu kuipokea na taarifa za kuharibika kwa mashine hiyo.

Anasema ni wajibu wa kila mfanyabiashara kutoa risiti huku wateja nao wakitakiwa kudai risiti baada ya kuhudumiwa kwa lengo la kujihakikishia kuwa kodi aliyolipa imefika sehemu sahihi.

Anaongeza kuwa mashine hizo zilianzishwa ili kuwasaidia wafanyabiashara kutunza kumbukumbu za biashara zao, kuwawezesha kujua kodi stahiki wanazotakiwa kulipa ikiwa ni pamoja na kuwezesha mapato ya serikali kufika yakiwa sahihi.

Anasema kwa mujibu wa sheria kila mwenye kipato anatakiwa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi kutokana na kuwa kodi ndio chanzo kikuu cha mapato ya serikali ambacho inakitegemea ili iweze kutekeleza majukumu yake katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Anasema kila mfanyabiashara anatakiwa kutumia mashine ya EFD ikiwa ni pamoja na kutoa risiti kila baada ya kufanya mauzo kwa mteja wake ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

Anaongeza kuwa kila mwananchi anatakiwa kuwa mzalendo kwa nchi yake kwa kulipa kodi kwa hiyari katika kila mapato anayopata ili kuiwezesha serikali kutekeleza jukumu la kufanya maendeleo katika jamii.

Anasema TRA imejiwekea mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inatanua wigo wa kukusanya kodi na mapato kuongezeka ili kuiwezesha serikali kupata kodi stahiki na ya halali kwa mujibu wa sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles