Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuweka mifumo imara ambayo itamtambua kila mfanyabiashara na bidhaa anayouza ili kuweza kukusanya kodi stahiki na kupunguza mianya ya ukwepaji kodi.
Dk Kijaji aliyasema hayo kwa viongozi wa TRA wa Mikoa ya Kodi ya Ilala na Kariakoo, wakati wa ziara yake ya kutembelea ofisi za mamlaka hiyo inayoendelea jijini Dar es Salaam.
Dk. Kijaji alisema TRA ina jukumu la kuhakikisha inavuka lengo la makusanyo iliyojiwekea ili kuweza kumsaidia Rais DK. John Magufuli, atekeleze majukumu yake kwa ufanisi na kulifikisha Taifa alipodhamiria.
“Naiagiza Mamlaka kuanza zoezi la kukagua watumiaji wote wa mashine za utoaji Risiti za Kieletroniki (EFD) hasa kwa wafanyabiashara wa Kariakoo ili kuhakikisha kila anayeuza anatoa risiti na anayenunua anadai risiti, kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza makusanyo na kusaidia Taifa kujiendesha kupitia fedha zetu wenyewe kwa kuwa hakuna Taifa huru bila mapato,’’ alisema Dk Kijaji
Aliwataka maofisa wa TRA kutokaa ofisini badala yake wawatembelea wafanyabiashara ili kuhakiki matumizi ya mashine za EFD.
Awali Meneja wa Ofisi ya Mkoa wa Kodi wa Kariakoo, Alex Katundu alimueleza Kijaji kuwa Mkoa wake wa una wafanyabiashara waliosajiliwa 22,279 na kati ya hao 16,068 wanatumia EFD.
Alisema Mkoa wa Kariakoo kwa mwaka 2018/19 walidhamiria kukusanya Sh bilioni 138.66 lakini walikusanya Sh bilioni 109 ambayo ni asilimia 79 ya malengo.
Katika Mkoa wa kikodi wa Ilala, Kaimu Meneja Steven Kuzeni alisema katika kuhakikisha mkoa wake unakusanya ipasavyo kodi ya majengo, wamedhamiria kusajili majengo yote yanayozunguka mkoa huo wa kikodi na hadi sasa wameshasajili majengo katika kata 26 kati ya kata 32 zilizopo katika eneo lake.
“Ofisi yangu kwa mwaka 2019/20 ina mkakati kabambe wa kuhakikisha inaongeza idadi ya walipa kodi ya mapato na wale wa Ongezeko la Thamani (VAT)” alisema Kuzeni.
Katika hatua nyingine Kijaji amewapongeza watumishi wa TRA kwa kuvuka lengo la makusanyo kwa mwezi Septemba ambapo imekusanya sh. trilioni 1.76.