30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

TRA kufanya zoezi endelevu kukagua mashine EFD Kariakoo

Na KOKU DAVID

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema itawashughulikia wafanyabiashara wote wa Kariakoo ambao sio waaminifu katika matumizi ya Mashine za Kodi za Kielektroniki (EFD).

Baadhi ya wafanyabiashara wanadaiwa kuwa na tabia ya kuzichezea mashine za EFD kwa lengo la kuiibia serikali kodi yake stahiki.

Hivi karibuni serikali kupitia wizara zake za Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ilikutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK) ili kujadili changamoto wanazokutana nazo katika biashara zao na kuangalia namna nzuri ya kuweza kuzitatua.

Katika mkutano huo ilielezwa kuwa maendeleo ya nchi hayawezi kupatikana bila ya kuwepo kwa wafanyabiashara hivyo viongozi wenye dhamana wanatakiwa kujiwekea utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara ili kujua changamoto wanazokutana nazo kutokana na mifumo ya kiutendaji serikalini ili zitatuliwe na serikali iweze kuendelea kupata mapato yake.

Pia ilielezwa kuwa miradi inayoendelezwa nchini inatokana na mapato ya ndani yanayotokana na kodi za wafanyabiashara hao.

Kamishna Mkuu wa TRA Charles Kichere ambaye alishiriki katika mkutano huo ikiwa ni pamoja na kukutana na uongozi wa wafanyabiashara hao katika ofisi za mamlaka hiyo anasema kuwa kila mfanyabiashara anatakiwa kutoa nyaraka za forodha zenye taarifa sahihi za  mizigo wanayoingiza nchini ili waweze kukadiriwa kodi stahiki.

Anasema ukweli wa taarifa utawawezesha kukadiriwa kodi stahiki ambayo haitamuumiza mfanyabiashara wala kuipunja serikali mapato yake.

Anasema hivi sasa muda wa kutoa mizigo umepungua tofauti na ilivyokuwa awali mizigo ilikuwa ikitumia muda mrefu hadi kutolewa bandarini.

Sambamba na hilo pia aliwataka baadhi ya wafanyabiashara wa Kariakoo ambao sio wazalendo kwa nchi yao kuacha tabia ya kuzichezea mashine za EFD kwa lengo la kutaka kuiibia serikali mapato yake.

Anasema kuwa TRA itakuwa ikitembelea katika maduka Kariakoo na kukagua mashine za EFD na kwamba watakaobainika kuzichezea mashine zao watachukuliwa hatua za kisheria.

Anasema hivi sasa mashine hizo zimetengenezwa katika viwango vya juu na kwamba tatizo la kuharibika mara kwa mara limekwisha hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kuacha kutoa visingizio vya ubovu wa mashine ili waweze kukwepa kodi.

Kichere anasema kuwa kila mfanyabiashara anatakiwa kuwa na mashine ya EFD pamoja na kutoa risiti kila baada ya kutoa huduma kwa mteja wake kama ambavyo sheria inamtaka kufanya.

Anasema mfanyabiashara mwenye changamoto katika biashara yake inayotokana na mifumo ya kiutendaji ndani ya mamlaka anatakiwa kutoa taarifa ili kuweza kuitatua na kumuwezesha kufanya biashara yake bila changamoto.

Anasema pia TRA itakuwa inawatembelea katika maeneo yao ya biashara wafanyabiashara mbalimbali ili kuweza kuwaelimisha kuhusiana na masuala mbalimbaali ya kodi ili kuepuka kumchukulia hatua mfanyabiashara ambaye atakuwa hana uelewa wa elimu ya kodi.

Anaongeza kuwa mamlaka hiyo imejipanga kuhaakikisha inatanua wigo wa kodi utakaoiwezesha kukusanya mapato hadi kuvuka lengo la serikali.

Anasema pia TRA imejipanga kuhakikisha inafanya kazi kwa ukaribu na wafanyabiashara ili kuiwezesha mamlaka hiyo kufikia malengo iliyojiwekea.

Kichere anasema wananchi wanatakiwa kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiyari ili kupuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

Anasema kwa mujibu wa sheria, kila mwenye kipato anatakiwa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles