Bakari Kimwanga, Dar es Salaam
Taasisi ya Tony Elumelu (TEF), imetangaza kufungua mzunguko wa tano wa Programu ya Wajasiriamali Afrika kuanzia Januari Mosi mwaka 2019.
Maombi hayo yatatumwa na kushughulikiwa kwenye kwenye jukwaa kubwa zaidi la mitandao kwa wajasiriamali wa Afrika.
Taarifa iliyotolewa na taasisi hiyo imeeeleza maombi hayo yataanza kupokelewa kuanzia siku hiyo, saa 12 asubuhi ambapo waombaji 1,000 waliochaguliwa wataunganishwa na wajasiriamali wengine wa sasa wapatao 4,470 katika programu hiyo.
“Tangu mwaka 2015, Mpango wa Biashara wa TEF – imekuwa ni kichocheo kwa wajasiriamali Afrika ambapo tayari imewawezesha wajasiriamali 4,470, ambao kila mmoja amenufaika kwa kupatiwa Dola 5,000 kila mmoja.
“Hatua hiyo huenda sambamba na mjasiriamali kuhudhuria mafunzo ya biashara yanayoendeshwa kwa wiki 12, ambao hupata ushauri na uzoefu na kujifunza zaidi mazingira ya Biashara ya Afrika,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, amesema wanufaika wa programu hiyo wamefanikiwa kuhojiwa kwenye vyombo vya habari vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na jarida la Forbes (Afrika).
Programu ya ujasiriamali imewezesha kubadilishana uzoefu kati ya wajasiriamali wa Afrika na viongozi wa sekta ya umma na wa kimataifa, wawekezaji na washirika wa maendeleo ya namna bora ya kuongeza biashara zao.
Sambamba na hilo pia wameweza kuongeza fursa na kuonyesha ubunifu wao na kutambua njia za kuimarisha mazingira ya biashara katika Bara la Afrika.