Na AVELINE KITOMARY, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) imekanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuwepo kwa dawa za Covifor na Jubi-R hapa nchini ambazo zinatajwa kutumika katika matibabu ya Covid-19.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo ilisema kuwa dawa hizo bado hazijasajiliwa kwaajili ya matumizi.
“Hivi karibuni kumekuwa na taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikihusisha dawa zenye kiambata hai (active ingredient) kinachofahamika kwa kitaalamu kama Remdesivir ambacho kimegundulika kuwa na uwezo wa kutibu ugonjwa wa Covid -19.
“Dawa hizo zenye viambata hai hiki zinajulikana kwa majina ya kibiashara kama Covifor inayotengenezwa na kampuni yenye jina Hetero Labs Ltd na Jubi-R inayotengenezwa na Jubilant Generics Ltd zote za nchini India.
“Dawa hizi za sindano zimefungashwa kwenye kifungashio ambacho lebo zake zinaonesha haziruhusiwi kusambazwa kwa nchi za Marekani ,Canada na Umoja wa Ulaya ambapo maandishi hayo yameleta taharuki na wasiwasi kwamba inawezekana dawa hizi zinazosambazwa maeneo mengine sio salama au duni na hazifai kwa matumizi yaa binadamu.
“Hivyo mamlaka inapenda kutoa ufafanuzi uandishi wa maneno hayo kwenye lebo ni wa kawaida kwenye sekta ya dawa ,”alibainisha.
Alisema kuwa lengo la maneno hayo ni kuzuia usambazaji wa dawa hizo kwenye nchi mbazo mtengenezaji au mgunduzi wa kwanza hajaruhusiwa kutokana na kuweka hakimiliki ya dawa yake.
“Dawa hii ya Redemsivir imegunduliwa kwa mara ya kwanza na kampuni ya jina la Gilead Ltd iliyoko nchini Marekani na imesajiliwa kwa dharura na mamlaka ya udhibiti wa dawa na chakula nchini Marekani(US-FDA) kwaajili ya kutibu Covid-19.
“Utaratibu huu unatumika kuidhinisha na US-FDA kwa dawa ambazo tafiti zake hazijakamilika ipasavyo kabla haijaruhusiwa rasmi kutumika kwa binadamu ili kuzuia na kutibu magonjwa yanayoambukiza kwa kasi na kusababisha vifo ikiwa kama hamna dawa nyingine kama ilivyo kwa Covid-19,Ebola na mengine.
“Kwa mantiki hiyo dawa zilizotajwa hapo juu zinatengenezwa na makampuni hayo mawili ya India baada ya kupewa kibali maalum na kampuni ya Gilead Ltd kwaajili ya kutengeneza dawa za genesi ili ziweze kutumika kwenye nchi zingine 127 duniani kwa mujibu wa makubaliano tofauti na nchi za Marekani,Canada na EU,”alifafanua.