MKURUGENZI wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi, amesema utabiri wao kwa mvua za vuli mwaka jana, ulikuwa sahihi kwa asilimia 91.7 ya matarajio.
Akizungumza katika mkutano na wadau wa TMA na wanahabari Dar es Salaam jana, Dk. Kijazi alisema kiwango hicho kinatokana na tathmini ya utabiri wa mvua hizo za vuli kwa Oktoba, Novemba na Desemba mwaka jana.
“Wakati tukielekea kupokea hali ya mvua za masika zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni, tathmini inaonyesha kuwa tumefanya vizuri katika utabiri wetu wa mvua za vuli za mwaka jana,” alisema Dk. Kijazi.
Alisema mamlaka hiyo inatambua madhara yatokanayo na hali mbaya ya hewa, hivyo imekuwa makini kuhakikisha taarifa zinawafikia wadau wote ili kuchukua tahadhari mapema.
Dk. Kijazi alisema Serikali pia imekuwa ikijitahidi kuijengea uwezo mamlaka hiyo kadiri iwezekanavyo, ili iweze kutekeleza majukumu yake na watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wazipate mapema na kufanya maamuzi sahihi kwa wakati mwafaka.
“Mamlaka pia inatambua madhara yaliyotokana na hali mbaya ya hewa katika maeneo mbalimbali hapa nchini hivi karibuni.
“Madhara hayo ni kama vile mafuriko yaliyozikumba kaya mbalimbali katika Mkoa wa Lindi na maeneo mengine nchini.
“Mamlaka inatoa pole kwa wote walioathirika na mafuriko hayo na kuwaomba Watanzania wote wawe wanafuatilia taarifa za hali ya hewa na tahadhari zinazotolewa na TMA ili kupunguza athari zinazoweza kutokea.
“Ninaendelea kusisitiza jamii kuwa bega kwa bega na TMA na kuepuka tabia ya kuwa na mazoea ya misimu ya hali ya hewa iliyozoeleka huko miaka ya nyuma, hasa ikizingatiwa kwamba mabadiliko ya tabia nchi yana athari katika mifumo ya hali ya hewa na hivyo kubadilika kwa misimu,” alisema Dk. Kijazi.
Alisema msimu unaokuja wa mvua za masika Machi hadi Mei 2020 ni wa mvua katika baadhi ya maeneo nchini, hasa yale yanayopata misimu miwili ya mvua.
Dk. Kijazi alisema kutokana na uhakika wa kuwapo kwa mvua, msimu huo pia ni wa kilimo katika maeneo hayo, hivyo ni muhimu wananchi na watumiaji wengine wa taarifa za hali ya hewa kupata taarifa sahihi na kwa wakati ili kuweza kujipanga na kujiandaa kabla ya msimu kuanza.
“Ili kufanikisha hilo, mamlaka imekuwa ikihakikisha inakutana na wanahabari ambao ni daraja muhimu katika kuwafikia wananchi wote kwa ujumla, ili kupata uelewa wa pamoja na namna bora ya kusambaza taarifa za hali ya hewa,” alisema Dk. Kijazi.
Alisema pamoja na kuangalia mwelekeo wa mvua za masika kwa kipindi cha mwezi Machi hadi Mei 2020, wataalamu pia wameandaa rasimu ya mwelekeo huo na viashiria vilivyosababisha kupatikana kwa utabiri wa hali ya hewa kwa msimu huo.
Dk. Kijazi alisema mamlaka hiyo inaendelea na juhudi za kuhakikisha taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinawafikia walengwa ikiwamo jamii kwa uhakika, usahihi na kwa wakati.
“Taarifa za hali ya hewa zikiifikia jamii kwa wakati, uhakika na usahihi itaisaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, pia itazisaidia mamlaka zinazohusika kupanga mipango endelevu ambayo haiwezi kuathiriwa na hali mbaya ya hewa,” alisema Dk. Kijazi.
Aliongeza kuwa TMA ni ofisi pekee iliyopewa jukumu la kutoa huduma za hali ya hewa kwa jamii hapa nchini.
Mamlaka hiyo inahusika kutoa tahadhari za majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa yanayoathiri sana watu na mali zao.
Majanga hayo huleta changamoto kubwa kwa wananchi, hususan wakulima, wavuvi, wafugaji na wasafirishaji.