Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanznaia (TMA) ,imetoa tahadhari ya kuwapo kwa vipindi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24 kati ya Januari 18 na 20 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam jana na mamlaka hiyo, ilisema maeneo yatakayoathirika na mvua hiyo ni pamoja na mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Kisiwa cha Unguja.
Taarifa hiyo ilisema hali hiyo inatokana na kuimarika kwa mgandamizo mdogo wa hewa katika eneo la Bahari ya Hindi mashariki mwa kisiwa cha Madagascar na hivyo kusababisha ongezeko la unyevunyevu kutoka misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuelekea katika maeneo hayo.
“Kutokana na kitendo hiki,wakazi wa maeneo haya tuliyoyataja pamoja na mamlaka zinazohusika na maafa tunawashauri kuchukua hatua stahiki na TMA tunaendelea kufuatilia hali hii na tutatoa mrejeo pale itakapobidi,” ilisema taarifa hiyo.