26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

TLS yaendesha mafunzo kwa Makundi Maalum kuhusu umuhimu wa Katiba Mpya

Na Grace Mwakalinga, Mtanzania Digital

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeanza kampeni ya kuwajengea uwezo makundi mbalimbali ya jamii, yakiwemo wenye ulemavu, wanafunzi wa vyuo, na wanawake, juu ya umuhimu wa kupata katiba mpya.

Katika jitihada za kufanikisha lengo hili, TLS inaendesha mijadala ya wazi inayotoa fursa kwa makundi haya kujadili mapungufu na mahitaji yao ili yaweze kuzingatiwa kwenye katiba mpya, ambayo inatarajiwa kukidhi mahitaji ya wananchi wote.

Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Mariam Othman, alitoa maelezo haya wakati wa mafunzo ya siku mbili yaliyoanza leo Juni 13,2024 yakihusisha makundi maalum na wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya Dar es Salaam.

Amesema kuwa TLS ipo tayari kukusanya maoni na kuheshimu mawazo ya kila mmoja bila kujali itikadi za kisiasa, kidini, au kijamii, kwani kila mmoja ana mchango muhimu katika upatikanaji wa katiba mpya.

“Lengo kuu la kuanzisha mijadala hii ni kuongeza ushirikishwaji wa wananchi kueleza masuala wanayohitaji ili yaingizwe kwenye katiba mpya,” alisema Mariam na kuongeza kuwa:

“Tumeanza kuendesha mijadala kuhusu katiba mpya mwanzoni mwa mwezi huu, ambapo tayari tumetoa mafunzo katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, na Dodoma, kwa kuyafikia makundi maalum, wanawake, viongozi, na wanafunzi wa vyuo ili kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko ya katiba mpya,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya katiba, Deus Kibamba, alieleza kuwa watu wenye ulemavu wanayo nafasi ya kuainisha masuala mbalimbali wanayoyahitaji ili yaingizwe kwenye katiba mpya, yakiwemo maboresho ya miundombinu kwenye taasisi za umma na marekebisho ya sheria kwenye katiba ya sasa kuhusu kundi hilo.

“Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) ni chombo muhimu ambacho kitaisaidia serikali kukusanya maoni mbalimbali ya wananchi kuhusu masuala ya kisheria na mambo ya kuingizwa kwenye mchakato wa katiba mpya,” amesema Kibamba na kuongeza kuwa:

“Marekebisho ya mara kadhaa yamefanyika kwenye katiba yetu tangu ilipoandikwa mwaka 1977, 1984, na 2005. Sasa imekuwa na viraka, maisha yanabadilika na kuna mambo ambayo yamepitwa na wakati, yanahitajika mengine kuingizwa kulingana na utu, haki, na mazingira ya wananchi,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Watu Walioumia Uti wa Mgongo, Abdulazizi Shambe, amesema baadhi ya huduma na mahitaji hawapati kwenye maeneo ya kutolea huduma, hivyo anaamini kupitia maoni aliyoyatoa yataingizwa kwenye katiba mpya.

Diana Pallangyo, mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Biashara (CBE), amesema miongoni mwa mambo yanayopaswa kushughulikiwa ni suala la wananchi wa Tanzania Bara kupata uhalali wa kumiliki ardhi Tanzania visiwani Zanzibar.

“Kwa mujibu wa Katiba ya sasa, imeainisha kuwa mtu wa Zanzibar anayo haki ya kumiliki ardhi Tanzania Bara wakati mtu wa Bara haruhusiwi kumiliki visiwani Zanzibar, jambo ambalo limekuwa likiibua mjadala na kuhitaji katiba mpya kuboresha eneo hilo,” amesema Diana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles