28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Deni la Taifa lafikia trilioni 90, Serikali yataja sababu kuongezeka

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema hadi kufikia Machi 2024 deni la Serikali limefikia Sh trilioni 90 lakini nchi bado iko imara kutokana na tathmini iliyofanywa na wataalam wa kukagua madeni.

Akizungumza leo Juni 13,2024 wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/2025 amesema kati ya deni hilo Sh trilioni 60 ni la nje na Sh trilioni 30 ni la ndani.

Amesema kutokana na kuchafuka kwa uchumi wa dunia kumesababisha bila mkopo wowote deni kuongezeka kwa zaidi ya Sh trilioni 5.

Kwa mujibu wa Dk. Nchemba sababu zingine za kuongezeka kwa deni hilo ni kutokana na mikopo ya zamani na mikopo mipya ambayo imeelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli ya kisasa, viwanja vya ndege na miradi ya umeme.

Vilevile kupungua kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2024 ambapo imeshuka kutoka 2300 hadi 2500.

“Madeni yanalipwa na yanapimwa, mara kwa mara tunajadili ongezeko la deni bila kutaja sababu zake na bila kutaja fedha hizo zimetumika wapi, ni kweli deni limeongezeka lakini ni vizuri tukajielekeza sababu za kuongezeka kwa deni na fedha hizo zimetumika wapi.

“Kwa muktadha huu ni muhimu kuelewa sababu za kuongezeka kwa deni, tumekopa Sh bilioni 17,000 kutoka nje kugharamia miradi na hizi zimeongeza deni, tunatakiwa tujadiliane kwamba miradi tuliyofanya kama haikuwa na tija…waliozoea kupita kwenye barabara nzuri wanaweza kuona umuhimu wa kukopa,” amesema Dk. Nchemba.

Waziri huyo wa fedha amesema pia wametoa hati fungani maalumu Sh trilioni 2.17 zilizotolewa kulipa mifuko ya hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma.

Amesema kwa mwaka 2024/2025 Serikali imepanga kukopa Sh trilioni 6.6 kutoka soko la ndani ambapo kati ya hizo Sh trilioni 4.2 zitatumika kulipa hati fungani zilizoiva na Sh trilioni 2.6 kugharamia miradi ya maendeleo.

“Watanzania wasitiwe hofu kwenye masuala ya deni, wataalamu wa kukagua masuala ya madeni ambao wameifanyia tathmini nchi yetu wamesema bado iko imara kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),” amesema.

Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali inatarajia kutumia Sh trilioni 49.35 kwa ajili ya matumizi, Sh trilioni 11 mishahara na Sh trilioni 2.17 kwa mfuko wa reli, barabara, maji, Rea na Tarura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles