NA CHRISTOPHER MSEKENA
MUZIKI hauna mipaka ndio maana tumeendelea kushuhudia vipaji vingi kutoka katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati vikisambaa duniani kote na kuendelea kufanya muziki wenye vionjo vya kiafrika.
Swaggaz leo tunakukutanisha na TITOK.O, mwanamuziki kutoka Sydney, Australia ambaye hivi karibuni ameingia kwenye chati za muziki Tanzania kupitia ngoma yake, DEKO aliyomshirikisha Dully Sykes.
Swaggaz: Kwa ambaye hakufahamu, TITOK.O ni nani?
TITOK.O: Kwa majina halisi naitwa Tito Malula aka TITOK.O au Real T ni mzaliwa wa Kongo DRC huko Kinshasa. Baba alituleta Tanzania, Dar es Salaam pale Magomeni Mapipa alikuja kimziki maana yeye amepiga muziki bendi na akina marehemu Remmy Ongala, Ndanda Kasheba, King Kiki na wengine wengi kuanzia miaka 1989 hadi 1996 na jina lake no Manesi Baba Malula.
Kwahiyo muziki ilikuwa kawaida kuingia maana kipaji nimetoa kwa baba na kuwasikiliza wakifanya mazoezi kila siku nyumbani.
Swaggaz: Changamoto zipi unazipata kufanya muziki nje ya Afrika?
TITOK.O:Â Changamoto ni nyingi, moja na prodyuza wanaojua staili zetu hawapo, gharama, watunzi hawapo, ma directors wa kufanya video nzuri hawapo, maana staili za chupa za wazungu ni tofauti sana na zetu nyumbani.
Ya mwisho ni sapoti au ‘sponsorship’ haipo maana hawaelewi lugha na hawana mawasiliano na waandaaji wa matamasha na matukio ya burudani.
Swaggaz: Bongo kuna wasanii wengi, kwanini ulichagua kufanya ngoma na Dully Sykes?
TITOK.O:Â Dully ni mzaramu mwenzangu (anacheka), Dully amekuwa kwenye Bongo Fleva kwa muda mrefu na ameendelea kuwepo kwenye kizazi kipya cha Bongo Fleva hii ni kitu spesho sana.
Nilikutana naye mwaka wangu wa kwanza kurudi Bongo 2015 na tukafanikiwa kufanya hit yetu ya DEKO 2019, nilitaka nionyeshe heshima ya kipaji chake ndio maana nikaamua kufanya naye kazi.
Swaggaz: Tabia gani ya mastaa wa Bongo inakuudhi linapokuja suala la kazi?
TITOK.O: Ya kwanza ni kukopiana yaani kila mtu anataka aimbe kama fulani. Ndio maana nilimchagua Dully Sykes Kwa sababu ana sauti yake mwenyewe ‘unique’.
Wasanii wengi Bongo wanapotea kwa sababu wanataka kuimba kama Kiba na Kiba yupo, promota watakupa vipi shoo wakati Kiba mwenyewe yupo.
Pili dharau, wasaani, prodyuza, waandishi wa habari, promota kama wewe sio Diamond, Burna Boy au Chris Brown hawana stori na wewe wanasahau kwamba hata hao wakubwa walianzia chini kwahiyo wanachukua hela yako na hawafanyi kazi.
Swaggaz: Muziki ni gharama, unatumia njia ipi kuhakikisha unaendelea kutoa ngoma kali?
TITOK.O: Muziki kweli leo hii ni gharama sana. Kuingia studio, lazima ulipe waandishi wasaidizi, prodyuza, video, kufanya wimbo upatikane mitandao zote za muziki unalipia hela, kuipromoti hela.
Kwa hiyo mimi nina studio nyumbani inayonisaidia na kuniruhusu kufanya demo kama zote. Kwa ufupi nina nyimbo zaidi ya 100, demo tayari kupeleka studio kubwa na kuziachia. Nafanya kazi kila siku ili ni sapoti muziki wangu maana sina meneja, ‘sponsors’ wala lebo inayonisimamia.
Swaggaz: Baada ya kuachia DEKO kitu gani kipya mashabiki watarajie?
TITOK.O: Deko ni moja ya nyimbo iliyo ndani ya EP yangu ya AUTHENTIC yenye ngoma sita zingine kali sana hadi wasanii wengine wameniomba tufanye kolabo baada ya kuisiliza walipoingia studio ya prodyuza mkali Kimambo aliyerekodi EP nzima.
 Wasanii ni wengi natamani kufanya nao kazi wa kike na wa kiume, siwezi kutaja majina maana nitajibana yeyote atakayejisikia kwamba mtindo wangu anauelewa nami naelewa yake, tutafanya kazi.
Swaggaz: Kwenye muziki ‘role model’ wako ni nani?
TITOK.O: Wa kwanza ni baba yangu mzazi, Papa Wemba,Koffi Olomide na Jah cure wa Jamaica.
Swaggaz: Sababu gani zinafanya utangaze muziki wako Afrika Mashariki hasa Bongo?
TITOK.O:Â Sababu ya kwanza nilimisi my second home, mimi nyumbani ya kwanza ya kuzaliwa ni Kinshasa, Kongo ya pili ya kujifunza uhuni pale Mzimuni shule zetu za kayumba Dar es Salaam na ya tatu ni hapa Sydney Australia.
Na kurudi Tanzania ilikuwa uchaguzi wa urahisi mno maana nilitoka DRC nikiwa mdogo sana, nimekulia my teenage life nimepitia Dar es Salaam kwahiyo kumbukumbu ziko nyingi mno na nnapenda kuimba kwa lugha ya Swahili japo kuwa ninaweza ya Kikongo kidogo.
Na mziki wa kizazi kipya umefikishwa mbali kote duniani kwa kishindo sana na wasaani kama Diamond Platinumz, Alikiba, Vanessa Mdee, Nandy na wengine wengi ndio maana najitangaza Afrika Mashariki na lazima nitaenda dunia nzima.
Swaggaz: Jambo gani lipo kwenye tasnia ya burudani hulipendi?
TITOK.O: Jambo lingine linalonisumbua sana kwenye ‘industry’ ya mziki wa Bongo ni swala la timu Clouds na timu Wasafi. Inaua muziki na vipaji kabla hata haijafanikiwa zaidi, yaani msanii mchanga ana ‘role model’ wake kama Maua Sama na anampenda pia Zuchu, sasa anapata kipengele cha kuchagua nani ashirikiane naye hata kabla hajafanya nao wimbo. Nadhani hilo bifu halina maana wanahitaji kuwa sawa kwa wasanii wote.