24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Tigo kupunguza wafanyakazi wake

Tigo-Tanzania-General-Manager-Diego-Gutierrez-copy

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Tigo imetangaza kupunguza baadhi ya wafanyakazi  waliopo katika kitengo cha Tigopesa kutokana na agizo  la Benki Kuu(BoT) kutaka kampuni mama ya mtandao huo (MIC) kuunda chombo kitakachosimamia biashara hiyo.

Tigo Tanzania ni kampuni tanzu ya MIC inayofanya biashara ya mitandao  ya simu katika nchi mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja Mkuu wa Tigo nchini Diego Gutierrez  kwa wafanyakazi, inaeleza; “Kutokana na Sheria ya Mfumo wa Malipo wa Taifa ya mwaka 2015 pamoja na mkutano uliofanyika hivi karibuni kati ya MIC Tanzania Limited  na BoT tungependa kuwahakikishia kuwa kampuni ya MIC kisheria inatakiwa kuunda    chombo kinachojitegemea  ambacho kitakuwa kinaendesha biashara yote ya Tigo pesa,”

Hata hivyo kampuni hiyo ilisema inafanya juhudi kuhakikisha wafanyakazi watakaopunguzwa wanapatiwa ajira nyingine katika mfumo mpya utakaokuwa ukiendesha biashara ya tigo-pesa.

Katika taarifa yake hiyo, Gutierrez  alisema hivi sasa wapo katika hatua ya kuanzisha mfumo huo mpya chini ya maelekezo ya BoT.

Pia alieleza kuwa wao kama kampuni watakwenda kufanya vikao vya mashauriano na wafanyakazi ambao wataathirika kutokana na mfumo huo mpya na kwamba miongoni mwa mambo ambayo watayajadili ni pamoja na  sababu ya kupunguzwa kwao.

Mambo mengine ni pamoja na hatua za kuchukua kuzuia  au kupunguza idadi ya watakaochishwa kazi, njia ya kuchagua wafanyakazi wa kuwapunguza, muda na malipo ya watakokumbwa na panga hilo.

Gazeti hili liliasiliana na Ofisa mmoja wa Tigo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini ambaye  alithibitisha kuwa tamko hilo ni la kwao.

Ofisa huyo alisema bado mazungumzo yanaendelea kati ya BoT na MIC ili kuweza kufanikisha zoezi hilo.

Zaidi alisema tangazo hilo limetolewa ili kukidhi vigezo vya kisheria vya kuwapunguza wafanyakazi wake.

Hata hivyo alisema idadi ya watakaopunguzwa bado haijajulikana na akamtaka mwandishi wa gazeti hili kufika katika ofisi za kampuni hiyo na kuonana na Meneja Rasilimali watu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles