Mke atibua ndoa ya mhadhiri, mwanafunzi wake

eee
Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Arusha, Martin Chamliho akifunga ndoa na mkewe flora Assey katika kanisa la Mtakatifu Theresia mkoani Arusha mwaka 2009.

 

NA FLORIAN MASINDE, DAR ES SALAAM

KATIKA hali isiyo ya kawaida, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Arusha (UoA), Martin Chamliho, amepigwa na butwaa baada ya mke wake wa ndoa, Flora Asei, kutinga katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva, kuzuia ndoa aliyopanga kuifunga kwa siri na Saum Rajab.

Martin ambaye ni mkazi wa Arumeru mkoani Arusha, alifika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufunga ndoa na Saum ambaye ni mkazi wa Kigamboni, Manispaa ya Temeke na taarifa zinasema alikuwa mwanafunzi wa chuo hicho.

Baada ya MTANZANIA Jumamosi kupata taarifa za kuwepo kwa tukio hilo, lilifika ofisi za wilaya hiyo ili kushuhudia na kukuta wanandoa hao wameshaondoka eneo hilo ndipo walipoamua kumtafuta ofisa aliyetakiwa kufungisha ndoa hiyo ambaye ni ofisa utumishi aliyekataa kutaja jina lake.

Ofisa huyo alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema yeye hana mamlaka ya kulisemea kwa kuwa ni suala la watu binafsi na kuomba watafutwe wahusika ili walisemee wenyewe.

“Binafsi siwezi kulizungumzia hili jambo kwa kuwa ni watu binafsi zaidi na mwenye mamlaka hayo hapa ni mkuu wa wilaya vinginevyo muwatafute hao wahusika wawaeleze nini kimetokea na kwanini,” alisema ofisa huyo.

Baada ya maelezo hayo, MTANZANIA Jumamosi lilifanya mawasiliano na wahusika kwa msaada wa shuhuda na kwa kupitia simu ya mkononi Martin alisema yeye hawezi kulizungumzia kwa kuwa anaye msemaji wake na kwa sasa yuko katika kikao maalumu hawawezi kuongea zaidi.

“Mimi siwezi kuongelea suala hilo, ninaye msemaji wangu na ikifika wakati wa kuliongelea ataongea ila kwa sasa tuna vikao muhimu nitawatumia namba yake baadaye naomba mtuache tafadhali,” alisema Martin.

Akizungumza na gazeti hili baada ya tukio hilo mke wa ndoa wa Martin, Flora alisema hana tatizo na mume wake na wana miaka nane katika ndoa hiyo.

Alisema walifunga ndoa hiyo mwaka 2009  katika Kanisa la Mtakatifu Teresia lililopo mkoani Arusha na baada ya hapo alipata nafasi ya kwenda kusoma Shahada ya Uzamili ya Mabadiliko ya Tabianchi nchini Australia kwa kipindi cha miaka miwili na kumuacha mumewe akiendelea na majukumu yake chuoni hapo.

“Mume wangu ambaye ni mzaliwa wa Mara wilayani Bunda, nilimucha nchini nakwenda kusoma nje ya nchi, lakini nilipofika kule nilimuita aje kunitembelea hapo ndipo nilianza kuona mabadiliko toka kwake kwa sababu hakuwa na utulivu kabisa.

“Ilifikia wakati anatoroka bila kujua na kulazimika kumtafuta hadi nafikia hatua ya kutoa taarifa polisi na hii ilisababisha pia kuomba msaada kwa ndugu kuona ni jinsi gani wangeweza kutatua hali hiyo,” alisema Flora.

Aliendelea kusema kuwa wakati akiendelea na masomo yake alikuwa anamtumia fedha kwa ajili ya kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo lakini mume wake alikuwa akizitumia kinyume na matarajio na  kumgharamia masomo Saum na kujenga nyumba kwa siri maeneo ya Maji ya Chai wilayani Arumeru.

Pia alisema baada ya kufanya uchunguzi aligundua kuwa mume wake na Saum walikuwa na uhusiano wa siri hadi kufikia hatua ya kuishi pamoja.

Alisema alipoamua kufuatilia sehemu walipokuwa wakiishi alikamatwa na polisi kwa maelezo kuwa ameenda kuwafanyia fujo.

“Kwa kweli nimevumilia mengi hadi nimewekwa lupango kwa ajili ya jambo hili, pia kinachoniuma ni fedha zangu zilizotumika kujenga nyumba hiyo na kumsomesha huyo binti inauma, nampenda mume wangu na nitazidi kupambana ili arudi kwangu kwa kuwa Mungu ndiye aliyenipa,” alisema Flora.

Kutokana na hali hiyo, aliamua kufungua kesi ya madai ya kuibiwa mume katika Mahakama ya Mwanzo Arusha ambayo inaendelea hadi sasa na kuweka pingamizi katika ofisi zote za wakuu wa wilaya za Temeke, Kinondoni na Ilala ili kulinda ndoa yake.

Kwa mujibu wa watu wa karibu wa Saum, kabla ya ndoa hiyo kutaka kufungwa, ndugu zake walijumuika kwa ajili ya sherehe ya jikoni maarufu kitchen party katika ukumbi wa Navy Beach uliopo Kigamboni wakati shughuli ya kumuaga ilitakiwa ifanyike leo katika moja ya ukumbi uliopo Kigamboni.

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Saum ambaye ni mkazi wa Kigamboni na alikuwa akisoma chuo hicho na kumaliza shahada ya elimu na kwa sasa ni mwalimu katika Shule ya Sekondari Nshupu iliyoko wilayani Arumeru lakini hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here