Na Hadia Khamis, Mtanzania Digital
Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) kimewashauri Watanzania wameshauriwa kuendelea kuwekeza nchini ili kuongeza pato la Taifa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika maonyesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba Afisa Forodha wa Kituo cha Uwekezaji(TIC), Leonard Mapunda amesema Serikali inaendelea kufanyia kazi malalamiko yanayotolewa na wawekezaji wa nje na ndani ya nchi katika maeneo ya Kisheria na Sera za kikodi ambapo yamekuwa yakilalamikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Malalamiko hayo yanakuja kutokana na kubadilishwa kwa sheria za kikodi kila mwaka wa fedha hali inayowapelekea wawekezaji kushindwa kujipangilia vizuri majukumu yao,” amesema Mapunda.
Amefafanua kuwa TIC inaendelea kusaidia wawekezaji katika kuhakikisha wanaunganishwa na watu katika maeneo ya kuwekeza na mazingira rafiki kwao.
“TICÂ inatoa elimu kwa wawekezaji wa ndani na nje juu ya uwekezaji wa biashara katika sehemu mbalimbali nchini ikiwemo katika viwanja vya sabasaba,” amesema Mapunda.
Amesema elimu wanayoitoa ni pamoja na ile ya sheria za kodi,sheria zao pamoja na vivutio vya uwekezaji.
Ameongeza kuwa Mwekezaji anapokuwa na cheti hicho kinafanya kupeleka maombi kwa Kamishna wa Forodha ili kusudi aweze kusamehewa asilimi 75 ya kodi.
Ameongeza kuwa kazi kubwa ya Afisa Forodha ni kufatilia mchakato huo kwa Kamishna wa forodha mpaka hapo kibali kitakapotoka kwa Kamishina wa Forodha ili uwekezaji uendelee.
“Tunachowashauri wawekezaji watembelee ofisi zetu, Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara watawapa elimu mbalimbali juu ya kupata taarifa pia kutembelea katika ofisi zetu za TIC ili kujifunza mengi juu ya uwekezaji,”amesema.