*Chabainisha Mtanzania ana nafasi mara 10 zaidi ya kuwekeza
Na Clara Matimo, Mwanza
KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeanza kampeni yake ya siku 30 kuzunguka mikoa yote nchini kwa ajili ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, kutoa elimu na kuwahimiza Watanzania kuchangamkia fursa na vuvutio vilivyopo badala ya kukaa pembeni wakidhani uwekezaji ni kwa watu kutoka nje ya nchi pekee.
Kampeni hiyo imeanza leo Januari 8, 2024 mkoani Mwanza ikiongozwa na Mkurugenzi wa Kituo hicho, Gilead Teri na baadhi ya wajumbe wa bodi ya kituo hicho ambao wametembelea baadhi ya sehemu za uwekezaji kikiwemo kiwanda cha kuchakata na kusindika nyama cha Chobo kilichopo Usagara wilayani Misungwi.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mkurugenzi wa TIC, Gilead Teri, amesema awamu ya kwanza ya kampeni hiyo itatumia siku 30 ambazo watazunguka nchi nzima kuhamasisha Watanzania kuwekeza nchini na kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na taarifa kwani kwa sasa kuna unafuu na wamerahisishiwa vigezo kupitia sheria ya uwekezaji ya mwaka 2022.
Teri amesema katika kampeni hiyo sekta zote za uwekezaji zimepewa kipaumbele na Mtanzania atakayevutiwa kuwekeza anapaswa kufika ofisi za kituo hicho kila mkoa nchini, ofisi za maafisa biashara ngazi ya wilaya na mikoa ili kupata taarifa zaidi zitakazowasaidia kufanya maamuzi ya kuwekeza.
“Tuko hapa Mwanza kuanza safari ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani kwa kuhamasisha ushiriki wa Watanzania ili kunufaika na mageuzi ya uchumi yanayotokea nchini. Tumeanza Mwanza tutaendelea mikoa yote awamu ya kwanza tutatumia siku 30 kuzunguka mikoa yote kuhakikisha Kila mtanzania anafikiwa na taarifa.
“Ninachoweza kuwaambia Watanzania ni kwamba kwa sasa kuna urahisi zaidi wa kuwekeza na Mtanzania ana nafasi mara 10 zaidi na mazingira ya uwekezaji ni salama. Tunapongeza uwekezaji unaoendelea katika mkoa wa Mwanza na Kila siku unakua tutaendelea kutoa ushirikiano na kusaidia wawekezaji kwa kuonyesha fursa zilizopo,” amesema Teri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla, amesema kupitia kampeni hiyo ni fursa kwa wawekezaji wa ndani kuelewa kwamba Serikali imeimarisha mifumo ya taarifa, sheria na mazingira ya uwekezaji huku akikaribisha wananchi kuwekeza mkoani humo kwani fursa na vivutio ni vingi na Mwanza ijayo inafurahisha kwani ni ya kimkakati zaidi.
“Nimefurahi kwa sababu mahali popote kituo cha uwekezaji kikifanya kazi vizuri kinachochea uwekezaji na kinatoa taswira ya nchi kuvutia wawekezaji, kwahiyo mnafanya vizuri kwa kugeukia hamasa ya wawekezaji wa ndani, mnafanya vizuri na sisi Mwanza tunaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha kwa sababu sisi ni mkoa wa kimkakati.
“Hamjafanya makosa kuchagua hapa mmechagua kimkakati sisi tunaiona Mwanza miaka michache ijayo itakuwa namba moja kutokaTunaahidi tutaitisha kikao cha wadau kwenye halmashauri maafisa biashara, wakurugenzi mje mtoe semina nzuri mkiondoka muwe na mabalozi wazuri kwamba TIC siyo tu kituo kwa ajili ya wageni bali kwa wazawa pia, kwakweli naiona TIC ya kisasa ambayo inaweza kuibadilisha Tanzania,” amesema Makalla.
Naye, Mjumbe wa bodi ya TIC, Mahfudhi Maulid, amesema kupitia ziara hiyo wamepokea maoni na mapendekezo mbalimbali ambayo wanakwenda kuyafanyia kazi kukifanya kituo hicho kiwe cha kuaminika na kukuza ushindani kwani wanataka kuwa na ushindani na kinara ili kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.