25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tibaijuka: Mimi na Muhongo ni majembe ya JK

mtanzaniadaily.2indd

Asifiwe George na Ester Mnyika, Dar es Salaam,
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amesema hatojiuzulu kwa sababu kufanya hivyo si fasheni.
Pamoja na kauli hiyo, pia ameweka bayana kuwa yeye na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, bado wanategemewa na Rais Jakaya Kikwete katika kumsaidia kufanya kazi.
Kauli ya Profesa Tibaijuka imekuja siku chache baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kutokana na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akauti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mbali na hayo, waziri huyo alieleza endapo uchunguzi utafanywa na kubaini fedha ambazo ziliingizwa kwenye akaunti yake na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira si halali, basi yupo tayari kuzirudisha.
Akizungumza Dar es Salaam jana kuhusu kuhusishwa kwake na sakata la Akaunti ya Escrow, Profesa Tibaijuka alisema wanaodhani kwamba anatarajia kujiuzulu wanakosea kwani kufanya hivyo si kutenda haki katika dhana ya maendeleo.
Profesa Tibaijuka alisema anavishangaa baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa kumwita ‘Mama Escrow’ huku akiweka wazi na kujiita yeye ni ‘mama wa migogoro ya ardhi’ na si ‘mama wa migogoro ya Escrow’.
“Mlifikiri nimekuja kujiuzulu, kumbe ndiyo maana mmekuja wengi, sikuja kujiuzulu ng’o kwani sina kosa na siwezi kujiuzulu kwa ajili ya mchango wa shule. Nikijiuzulu nitakuwa sitendi haki katika dhana ya maendeleo na kujiuzulu siyo fasheni.
“Sijaja kujiuzulu wala kutetea watu wenye madhambi, pia uongo ukirudiwa mara nyingi unageuka na kuwa ukweli, kilichonileta hapa ni kufafanua lengo la fedha hizo ambazo zilikuwa za shule ingawa suala lenyewe linaonekana kuwa na utata.
“Fedha hizo zilitolewa na watu wenye nia njema ya elimu kwa watoto wa kike kwani kipindi hicho elimu yao ilikuwa katika kiwango cha chini tofauti na wavulana hali iliyoleta mvutano kuwa watafutiwe kiwango maalumu cha ufaulu.
“Wizi na uongo ni dhambi, tusiwe watu wa kuhukumu kwani ni dhambi ya mauti, sikuwahi kuitwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali inayoongozwa na Zitto Kabwe wala kamati yoyote kueleza suala hilo na nilishangaa kuona jina langu lipo kwenye orodha ya Escrow,” alisema Profesa Tibaijuka.
Katika mkutano huo, Tibaijuka alisisitiza kuwa anaona fahari kufanikisha mchango wa shule yake iliyoingiziwa fedha hizo, na kwamba aliyemfadhili aliweka masharti ya kufungua akaunti Benki ya Mkombozi pekee na kisha kuingiziwa kiasi cha Sh bilioni 1.617.
Aidha alisema maazimio yaliyotolewa na Bunge ya kutaka uchunguzi uendelee kufanyika, bado yamekuwa yakileta mkanganyiko kwani azimio namba tatu linataka waliohusika wawajibishwe.
“Nikijiuzulu hata Rais Jakaya Kikwete atanishangaa kwani fedha nilizopata ni za shule na kwa ajili kukomboa elimu nchini, hasa kwa watoto wa kike kutokana na wazazi wengi kutoweza kumudu gharama za shule,’’ alisema.
Alisema utata huo utaondoka kwa kutoa elimu kwa wananchi na endapo kuna suala lolote ambalo halikueleweka aliwataka wanahabari kumuuliza maswali mengine Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.
Waziri huyo alisema udalali wake wa fedha hizo ni kwa ajili ya wanafunzi katika shule za Taasisi ya Barbro Johansson Girls’ Education Trust ambazo zilitoka katika kampuni ya James Rugemalira kama msaada kwa shule hiyo.
Alisema udalali wake ni kutafuta fedha kwa ajili ya elimu nchini, ambapo alidai hata Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP , Dk. Reginald Mengi alitoa Sh milioni 248 kwa ajili ya msaada wa shule hiyo.
Profesa Tibaijuka alisema wananchi watambue yeye ni mstaafu wa Umoja wa Mataifa, hivyo hawezi kufanya hivyo na kama angetaka fedha hiyo angeweza kuzifuata hata katika shule na kuchukua.
Desemba 16, mwaka huu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye ni mmoja wa watuhumiwa katika kashfa ya Escrow alitangaza kujiuzulu.
Hatua hiyo ya Werema ilikuja wakati Watanzania wakiwa bado wanasubiri uamuzi wa Rais Kikwete kuhusu maamizio nane ya Bunge yaliyotokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyekagua miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika maazimio ya Bunge, baadhi ya viongozi ambao chombo hicho kiliona wana makosa na kutaka mamlaka zao za uteuzi ziwachukulie hatua, ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Tibaujuka, Jaji Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles