28.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

Mkono anusurika kutekwa Dar

mkonobcNa Kulwa Karedia

MBUNGE wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), amesurika kutekwa na watu wasiofahamika katika eneo la Tangibovu, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa na Mkono mwenyewe, ilisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4:30 asubuhi.
“Nikiwa na wasaidizi wangu wawili tukitoka Bagamoyo tukiwa ndani ya gari langu aina ya Marcedes Benz katika eneo la Mbezi Tangibovu ghafla yalitokea magari mawili ya Toyota Prado na Toyota Land Cruiser VX na kufunga njia.
“Lakini dereva wangu baada ya kuona hali hiyo aliamua kuondoa gari na kupitia pembeni na kufanikiwa kutoka eneo nililokuwa nimezuiliwa,” alisema Mkono.
Alisema baada ya kutoka eneo hilo, magari hayo mawili yaligeuza na kumfuata yakiwa mwendo kasi.
“Baada ya kutufikia tena, kijana mmoja akiwa amevalia miwani nyeusi ndani ya gari la Land Cruiser VX alishusha kioo na kutuamuru tusimamishe gari langu.
“Katika hali hii, dereva wangu alitoa gari kwa kasi hadi njia panda ya Kawe ambako tulimkuta askari polisi aliyekuwa doria pembezoni mwa barabara, tukamweleza na kuomba msaada kwake,” alisema Mkono.
Alisema cha ajabu baada ya kuona wamesimama na polisi, magari hayo yalipita kwa kasi yakielekea eneo la Mbezi Beach.
“Askari yule alitushauri tukatoe taarifa Kituo cha Polisi Kawe kilicho karibu na nilipewa RB. Na KW/12156/2014.
“Kutokana na tukio hili, nilipata mshtuko na kumuomba msaidizi wangu anipeleke nyumbani kwangu Masaki kwa ajili ya kupumzika,” alisema Mkono.
Alisema tukio hilo limemfanya aendelee kuwa na hofu ya usalama wake kwani tayari anahisi watu waliofanya kitendo hicho wana nia mbaya na yeye na kuvitaka vyombo vya dola vichunguze tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alipoulizwa juu ya tukio hilo, alikiri kuwapo.
Alisema mtu mmoja ambaye ni dereva, David Katikilo, alifungua jalada kituo cha Kawe akisema juzi, wakati wakitoka Bagamayo akiwa na Mkono waliona magari mawili yaliyokuwa yakiwafuatilia.
Alisema tukio hilo lilitokea asubuhi, lakini mlalamikaji alitoa taarifa katika kituo cha polisi Kawe saa 10 jioni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles