26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

TIA yatakiwa kujaza wanafunzi kampasi zote

Na Mwandishi wetu, 

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu  Nchemba,  ameitaka Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kuweka mikakati ya kuhakikisha miundombinu iliyopo inatumika  na kampasi zote saba zinapata wanafunzi.  

Akizungumza leo Desemba 15,2023 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Fedha, katika Mahafali ya 21 ya TIA, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,  Elijah Mwandumbya, ameitaka taasisi hiyo kuweka mikakati  ili watanzania watumie fursa za kujiendeleza kielimu kupitia kozi mbalimbali zinazotolewa kwenye chuo hicho.

Amesema Serikali  imetumia gharama kubwa kujenga miundombinu hiyo, ikilenga kupunguza adha wakati wa uendeshaji wa shughuli za taasisi  na kuboresha utendaji katika utoaji  huduma. 

“Serikali inatumia fedha za watanzania kugharamia ujenzi wa miundombinu. Hakikisheni watanzania wanapata taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo kila mara, pamoja na masuala mbalimbali yanayofanywa na Serikali kupitia taasisi hii, ”amesema.

Ameagiza kuwa miundombinu iliyojengwa itunzwe ili idumu kwa kipindi kirefu na  kubaki katika hali ya ubora wa kutoa elimu kwa watanzania wote.

Aidha amewataka wafanye  kazi kwa bidii, uadilifu, ubunifu, umakini, weledi na kujiepusha na uzembe, kwa kuzingatia sera, sheria, taratibu na kanuni ili kujiimarisha zaidi na kushindana katika soko la ajira.   

“Lazima muendelee kujielimisha kwa lengo la kujenga ujuzi na maarifa ya kutosha, kadri inavyowezekana, ili muweze kutumikia Taifa kwa viwango vya hali ya juu,” amesema  Mwandumbya. 

Amefanua kuwa serikali itaendelea kushirikiana na TIA kuhakikisha kuwa wanaweza kukabiliana  na changamoto mbalimbali hasa zinazotokana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia,pamoja na ongezeko la idadi ya wanachuo.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya kusomea na kufundishia, katika kampasi za TIA kupitia wizara ya fedha.

Katika mahafali hayo  jumls ya wahitimu 7,222 wa kampasi ya Dar es Salaam, wakiwemo wanawake 3,957 na wanaume 3,269 walitunukiwa vyeti vya shahada mbalimbali.

Hata hivyo  jumla wahitimu kwa kampasi sita za chuo hicho ni 13,265, wakiwemo wanawake 7,155 na wanaume 6,110 isipokuwa  kampasi ya saba ya Zanzibar ambayo imeanza kupokea wanafunzi mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles