Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeuiomba Serikali kupitisha sera waliyoiunda na kutunga sheria inayowatambua na kuwalinda watetezi wa haki za binadamu nchini.
Akizungumza Julai 5,2024 wakati wa uzinduzi wa ripoti ya 11 kuhusu hali ya watetezi wa haki za binadamu na nafasi ya kiraia nchini, Mratib Taifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema kukosekana kwa sera na sheria kumesababisha watetezi wa haki za binadamu kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa mwaka 2023 watetezi 100 wa haki za binadamu walipata madhila mbalimbali na kusaidiwa kwa uhamisho wa muda mfupi, matibabu, msaada wa kisheria na usaidizi mwingine wa dharura ambapo 42 walipata usaidizi wa kisheria kutoka THRDC.
“Ukosefu wa sera na sheria kuhusu ulinzi wa watetezi wa haki za binadamu unaendelea kuwa changamoto katika kutekeleza majukumu yao, lakini licha ya serikali kutambua kazi za watetezi wa haki za binadamu hadi sasa Tanzania haina sera na sheria.
“THRDC inaamini kwamba serikali inayofanikiwa lazima ishirikiane na kuhakikisha nafasi ya kiraia kwa Azaki na sekta binafsi kwa ujumla hivyo, mazungumzo yaimarishwe ili kuwa na uhakika wa ulinzi wa haki za binadamu na watetezi katika siku zijazo,” amesema Olengurumwa.
Hata hivyo amesema mwaka 2023 Serikali ilionyesha dhamira katika kushirikiana na mashirika ya kiraia kukuza haki za binadamu na imechukua hatua za makusudi kuimarisha utawala wa kidemokrasia na kwamba kujitoa kwa serikali kunadhihirika kupitia mipango na mageuzi ya mfumo wa haki jinai.
“Tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Sita kuna maboresho ya mikutano ya kisiasa na mikusanyiko mingine muhimu ya asasi za kiraia…kuna changamoto za kutoheshimu utawala wa sheria na kutokuwa huru kwa mahakama,” amesema.
Aidha amesema wataendelea kutetea marekebisho ya sheria zenye vikwazo na kupigania kujumuishwa kwa haki na ulinzi wa watetezi wa haki za binadamu katika katiba ijayo huku akiziasa Azaki kujipanga upya ili kusukuma mageuzi ya sheria zinazowaathiri.
Mratibu huyo pia amemuomba Rais aunde tume itakayochunguza sheria za vyombo vya habari nchini na kupendekeza kwa serikali marekebisho ya sheria hizo.