25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

THE MAFIK USO KWA USO NA BABU SEYA, PAPII.

Na CHRISTOPHER MSEKENA


HABARI kubwa kwenye anga la burudani mjini ni shoo ya wakali wa dansi Bongo, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na Johnson Viking ‘Papii Kocha’, itakayofanyika leo kwenye Ukumbi wa King Solomoni, jijini Dar es Salaam.

Shoo hiyo ni ya kwanza tangu watoke jela baada ya kukaa kifungoni kwa miaka 14. Weka hiyo pembeni, unawakumbuka Yamoto Band? Ni zilipendwa, kwa sasa kundi hilo limevunjika na kila msanii anafanya kazi zake binafsi.

New brand town kwa sasa ni The Mafik, kundi lililopewa heshima ya kipekee leo kutumbuiza kwenye onyesho hilo la wakali, baba na mwana.

THE MAFIK NI NINI?

Kundi hili ambalo limefanikiwa kujizolea mashabiki wengi kupitia singo yake ya kwanza Passenger, linamikiliwa na uongozi mkubwa huku miongoni mwa washika dau wake wakiwa ni staa wa Bongo Fleva, Nurdin Bilal ‘Shetta’, Kapasta na Mx Carter meneja biashara aliyesimama nyuma ya mafanikio ya wasanii wengi akiwamo Aslay.

“Neno The Mafik lina maana ya bahati kwa hiyo wanaounda kundi hili wana bahati maana baada ya kufanya usahili ndiyo tukawapata hawa Rhino King, Hamadai na Mbalamwezi wanaounda kundi hilo na hii siyo bendi japo lina uwezo mkubwa wa kutumbuiza na vyombo vya muziki,” anasema Shetta alipozungumza na Swaggaz.

VIPI KUHUSU PESA, WANAWAKE?

Baada ya uzinduzi mkubwa wa The Mafik uliofanyika Februari 3, mwaka huu Club Next Door Masaki Dar es Salaam na mastaa mbalimbali kuhudhuria, picha iliyojengeka ni ile inayoonyesha hawana mipaka na hawafungamani na upande wowote.

“Kwanza kabisa wana mwaka mmoja na nusu tangu   wajuane, tumewanjenga, tumewapa mbinu ambazo zinavunja makundi mengi kwa sababu mara nyingi huwa ni pesa au wanawake. Tunaamini sisi tupo katika umoja na lengo ni kuwafikisha mjini The Mafik,” anasema Shetta.

MGAWANYO WA KAZI

Rhino King anasema kinacholitofautisha Kundi la The Mafik na wengine ni kwamba wasanii wake kuwa na uwezo mkubwa wa kuimba, kutunga na kucheza vyombo vya muziki, kitu ambacho ni adimu.

“Mbali na kutunga nyimbo mimi napiga ngoma na kupiga gitaa kidogo si sana, Mbalamwezi anapiga gitaa vizuri sana na Hamadai anapiga piano sana,” anasema Rhino King.

HAMADAI

Aliwahi kugonga vichwa vya habari za burudani alipokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Shilole, kuandika nyimbo za mastaa pamoja na nyimbo zake nje ya The Mafik kama vile Wangere, Marioo zilizofanya vizuri.

“Nilipotakiwa kujiunga na The Mafik nilikuwa na furaha kwa sababu nilikuwa nawafahamu wenzangu, nilifurahi sababu timu ambayo nafanya nayo kazi inajiweza,” anasema.

MBALAMWEZI

Anasema jina hilo alilipenda baada ya kujua nguvu ya mwezi kwenye giza kitendo kinachoitwa mbalamwezi.

“Nilikuwa sijui maana yake maana kabla nilishajiita majina mengi, nilipokuwa Mafia nilienda kuchukua samaki, muuzaji akaniambia wamepanda bei sababu ya mbalamwezi, akaniambia hawaonekani kwa sababu samaki ni ngumu kupatikana kwa sababu wanaona,” anasema.

RHINO KING

Anasema mbali na muziki ni mcheza soka katika dimba uwezo wake watu walimpa jina la Kifaru na alipoingia kwenye muziki akaamua kulitumia.

“Niliitwa Kifaru wakati nacheza soka kwa sababu ya nguvu zangu, nikalitoa kwenye Kiswahili na kuliweka kwenye Kiingereza likaja Rhino nilipoanza rasmi muziki ili liwe na swag,” anasema.

WALICHOJIFUNZA TAMASHA SAUTI ZA BUSARA

The Mafik walikonga nyoyo za mashabiki wao visiwani Zanzibar katika tamasha kubwa la Sauti za Busara lililofanyika Februari 8-11 mwaka huu katika ngome za Mji Mkongwe. Je wawamepata uzoefu gani baada ya kutumbuiza kwenye tamasha hilo kubwa Afrika Mashariki?

“The Mafik wapo kwenye familia kubwa, tukipata simu moja kwa moja kutoka kwa Fid Q kuwa The Mafik wanahitajika Zanzibar, sisi kama viongozi tukaona ni vizuri waende, ikawa hivyo ili wapate uzoefu kwenye majukwaa makubwa,” anasema Shetta.

USO KWA USO NA BABU SEYA, PAPII OCHA

The Mafik wanasema hii ni heshima kubwa kwao kupata nafasi ya kutumbuiza kwenye jukwaa moja na Babu Seya na Papii Kocha ikiwa ndiyo onyesho lao la kwanza linalotarajia kuhudhuliwa na mashabiki wengi.

“Kama kawaida yetu sisi ni watu wa ‘live band’ kwa hiyo kesho (leo) pale jukwaani tumepanga tuandike historia ya aina yake kama kundi pekee linalotumbuiza na kina Papii Kocha na Babu Seya,” anasema Hamadai.

 PAPII KOCHA ATOA NENO

“Hii ni shoo ambayo nilikuwa naiwaza kama ndoto hewa sababu nilikuwa sijui lini itatimia lakini kwa baraka za Mwenyezi Mungu na Rais Magufuli amefanya ndoto yangu iwe hai.

“Mimi na mzee wangu tutakutana na ndugu jamaa na mashabiki zetu kesho (leo) kwa mara ya kwanza baada ya kutoonana nao kwa miaka 14,” anasema Papii alipozungumza na paparazi wa Swaggaz.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles