23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

MARAFIKI WANAWEZA KUKUSAIDIA, KUKUANGUSHA KIMAISHA

Na ATHUMANI MOHAMED


KATIKA safari ya mafanikio marafiki ni kiungo muhimu. Marafiki wanaweza kukuvuta shati ukiwa kwenye kilele cha mafanikio lakini pia wanaweza kukupa moyo wakati umeanguka.

Marafiki wanaweza kukukatisha tamaa, lakini pia wanaweza kukupa mbinu za kuvuka kwenye vizingiti vizito vya mkwamo kimaisha. Tunaishi na jirani zetu, bila shaka kati yao, tumechagua watu wa kushirikiana nao.

Tunafanya kazi na marafiki zetu pia, lakini tunakunywa nao kahawa au mvinyo jioni mara baada ya kukamilisha majukumu yetu ya kikazi. Ni muhimu sana, kuliko kawaida.

Wakati fulani, tukiwa kwenye matatizo ya hapa na pale, inatupasa kuwashirikisha marafiki zetu ili watusaidie mawazo. Hapo sasa unaweza kuona nguvu ya marafiki katika maisha yetu ya kila siku.

Swali la msingi la kujiuliza ni je, unao marafiki wa aina gani? Je, wamekuwa msaada kwako kwa kiwango gani? Wamekuwa na majibu ya changamoto zako kwa kiwango gani?

Huenda kuna makosa mengi uliyafanya huko nyuma lakini ni makosa makubwa kuendelea kufanya makosa yaleyale kila mara.

Hii ndiyo sababu sasa nakupa aina za marafiki ambao hupaswi kuendelea nao kwa sababu wanaweza kukusababishia mkwamo wa kimaisha.

  1. WASIOSHIRIKIANA NAWE

Inawezekana unao marafiki na unawapenda, unawaheshimu na unajitoa sana kwao katika mambo mbalimbali iwe binafsi au kijamii.

Wao wakikuambia kuna ndugu yao anafunga ndoa, unatoa mchango na kuchukua kadi hata kumi kuwapatia marafiki zako wengine ili kufanikisha. Umekuwa mstari wa mbele wanapokuwa na matatizo ya kufiwa au kuuguliwa na pengine wengine kuugua.

Mara kadhaa umejitoa kwa ajili yake, hadi kufikia hatua ya kutoa damu kwa ajili ya kumuongezea ndugu yake ambaye mpo kundi moja la damu. Lakini kila ukimwangalia rafiki yako huyo, unagundua kuwa wewe ukiwa kwenye uhitaji hana msaada na wewe.

Ulimweleza kuhusu mke wako kulazwa Muhimbili, akaishia kukuambia: “Pole sana rafiki yangu, Mungu atakusaidia.”

Ulimweleza kuna ndugu yako anafunga ndoa, akaishia kutoa ahadi na mwisho wa siku hakuchanga chochote na hata kukusindikiza kwenye sherehe hakutaka. Rafiki anayejiangalia mwenyewe hana maana yoyote kwako.

Kama hana anachokusaidia, wa kazi gani? Fanya maamuzi magumu. Ni vyema kuachana kabisa na watu wa namna hiyo. Tulia tafuta marafiki wengine. Wapo tu.

  1. WANAOKUKATISHA TAMAA

Wapo jamaa ambao kazi yao ni kukatisha wenzao tamaa. Ni rafiki yako sawa, mnashirikiana kwenye mambo ya msingi sawa, lakini kila unapomshirikisha jambo fulani lenye masilahi kwako, anaishia kukuambia: “Aaah hiyo ngumu, hutaweza ndugu yangu. Waachie wengine. Hilo siyo jambo la mchezomchezo.”

Lakini ukija kufuatilia baadaye, unagundua kuwa wazo lile analifanyia kazi yeye. Huyo hakufai, maana anakurudisha nyuma kimaendeleo. Kuwa mwenye maamuzi magumu, lakini yenye manufaa kwako.

Ni wakati wako wa kuchuja kabisa rafiki zako, ubaki na wale wenye maana katika maisha yako. Wenye mchango kwako, wenye kushirikiana na wewe, ambao wanaweza kuwa chachu ya kukusogeza kwenye mafanikio.

Wiki ijayo tutaendelea katika sehemu nyingine. Nakutakia mema. Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles