30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TFF yacharuka Cannavaro kumnadi Magufuli

NADIR CANNAVARONA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limewapiga marufuku wanafamilia wake kuelezea hisia zao za kisiasa au kujihusisha katika kampeni za kisiasa wakiwa katika mavazi rasmi ya mchezo huo.

TFF imechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa vitendo vya wanafamilia wake kujihusisha na masuala ya siasa wakiwa katika mavazi rasmi ya mpira ambayo yana nembo za klabu na wadhamini wa ligi.

Mmoja wa wachezaji waliofanya kitendo hicho ni nahodha wa timu ya Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, aliyepigwa picha akimnadi mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli akiwa ameshika mpira, kipeperushi cha mgombea huyo na kuvalia jezi ya Yanga.

Katiba ya TFF Ibara ya I (4) inatamka: “TFF ina usawa kwenye mambo ya kisiasa na dini. Ubaguzi wa aina yoyote dhidi ya Taifa, mtu binafsi au makundi yenye uhusiano kwenye jamii, rangi ya ngozi, kabila, asili ya Taifa au kijamii, jinsia, lugha, dini, maoni ya kisiasa au mengine yoyote, utajiri, kuzaliwa au hadhi nyingine yoyote imepigwa marufuku na kuna adhabu ya kufungiwa au kufukuzwa.”

Pia kanuni za ligi, Kanuni ya 14 (40) inatamka: “Hairuhusiwi kwa mchezaji, mwamuzi au kiongozi wa timu kuonyesha kwa njia yoyote tangazo au ujumbe unaohusiana na dini yoyote au ulio na dhumuni maalumu bila idhini ya TFF au Bodi ya Ligi (TPLB).”

“TFF inachukua fursa kuwakumbusha wana familia wote wa mpira wakiwemo viongozi, wachezaji, waamuzi, makocha na madaktari wa michezo kuwa ni marufuku kuelezea hisia zao za kisiasa au kujihusisha katika kampeni za kisiasa wakiwa katika mavazi rasmi ya mpira zikiwemo jezi na track suites zenye nembo za TFF, klabu, wadhamini na ligi, Taifa Stars au za washirika wa TFF wakiwemo wadhamini,” alisema Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto.

Katika hatua nyingine, TFF imepiga marufuku mashabiki wa mpira kutumia fursa ya mechi za soka kubeba mabango au kusambaza ujumbe wa kisiasa, yeyote atayekiuka sheria hizo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Ikumbukwe kuwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) nalo limewahi kupiga marufuku mihemko ya ishara au maneno ya kisiasa, matangazo au udini kwa wachezaji kwenye jezi zao uwanjani na kuna baadhi ya wachezaji wameadhibiwa kutokana na hilo.

Mfano mwaka jana nyota wa Ufaransa, Nikolas Anelka, alifungiwa kutocheza mechi tano na faini ya Dola za Marekani 80,000 baada ya kuonyesha ishara ya kisiasa ya ‘quenelle’ wakati alipoifungia bao West Bromwich, ishara iliyotumiwa kama salamu na wafuasi wa Chama cha Nazi (Ujerumani) kilichokuwa kikiongozwa na Adolph Hitler.

Hapa Afrika mwaka juzi klabu ya Al Ahly ya Misri ilimfungia mchezaji wake, Ahmed Abdul Zaher na kumweka sokoni baada ya kumsapoti Rais wa zamani wa nchi hiyo aliyepinduliwa na jeshi, Mohamed Morsy kwa kushangilia bao kwa kunyoosha juu vidole vinne, ishara inayotumika na wafuasi wa Morsy.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles