Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), unatarajia kufanyika kesho, jijini Tanga ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili Kiomoni Kibamba amesema ikifika saa 9: 00 Alasiri, viongozi waliopita watakuwa wamejulikana.
Akizungumzia maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi leo, Kibamba amesema Agenda Kuu itakuwa ni uchaguzi na asilimia 90 ya wajumbe wamesawasili Tanga kutokana maeneo mbalimbali.
“Kwa kifupi maandalizi yote yamekamilika, uchaguzi utafanyika kesho tarehe 7, Agosti, niwaombe Watanzania kuwa watulivu kwani itakapofika saa tisa , watakuwa wamejua ni viongozi gani wamepata nafasi ya kuongoza mpira wetu kwa miaka minne,” amesema Kibamba.
Katika uchaguzi huo, mgombea wa nafasi ya Urais, Wallace Karia hana mpinzani, huku mpambano ukiwa kwenye kinyang’anyiro cha Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao kila Kanda wapo zaidi ya mmoja.