31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

TFF isiishie kwa Stars pekee, Serengeti Boys pia wapo

TANZANIA  itakuwa mwenyeji wa fainali za Vijana walio chini ya umri wa miaka 17, zitakazofanyika nchini mwakani, huku timu ya Taifa ya Tanzania ya umri huo, Serengeti Boys, ikishiriki michuano hiyo kwa mara ya pili.

Timu hiyo kwa mara ya kwanza ilishiriki michuano hiyo mwaka jana nchini Gabon, ambapo ilitolewa katika hatua za makundi, licha ya kuonyesha kiwango kizuri.

Safari hii Serengeti Boys itashiriki moja kwa moja michuano hiyo itakayofanyika nchini kutokana na kuwa mwenyeji, baada ya kupewa nafasi ya kuandaa fainali hizo na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), Mei mwaka 2015.

Hii ni fursa ya kipekee ya kuwa mwenyeji, lakini pia ni wakati wa Serengeti Boys kuitangaza vyema Tanzania kwa kuhakikisha inatwaa ubingwa huo katika ardhi ya nyumbani.

Serengeti Boys kwa sasa inasubiri muda pekee wa kushiriki fainali hizo, lakini Taifa Stars ipo kwenye mapambano ya nkuhakikisha inafuzu kwa Fainali za Afrika (AFCON), zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.

Timu zote hizo zipo katika majukumu mazito, wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Serikali, ikiwa katika mikakati ya kuhakikisha Stars inafuzu kwa fainali hizo, ipo haja pia ya kuhakikisha Serengeti Boys inatwaa kombe hilo kwa kufanya maandalizi ya uhakika.

Sisi MTANZANIA tunaunga mkono jitihada zinazofanywa ili Stars inafuzu kwa fainali za AFCON, lakini pia tunaiasa TFF isielekeze nguvu nyingi kwenye timu hiyo na kuisahau Serengeti Boys.

Ipo haja ya kuwekwa mikakati kwa Stars lakini pia kwa Serengeti Boys, ili kuhakikisha kuwa zote zinafanya vizuri na kuitangaza Tanzania katika medani ya kimataifa.

Stars kufuzu kwa AFCON itakuwa imerudisha furaha na faraja kwa Watanzania, ambao walikosa kushuhudia timu yao kwenye michuano hiyo, tangu ilipofuzu kwa mara ya kwanza mwaka 1980, mjini Lagos, nchini Nigeria.

Huu ni mwaka wa mapambano katika soka la Tanzania, ni wakati wa kuandika historia mpya katika soka la kimataifa, si wakati wa mgawanyiko wa Simba na Yanga, ni suala la umoja na mshikamano kwa watanzania wote.

Stars kufuzu AFCON mwakani nchini Cameroon na Serengeti Boys kutwaa ubingwa wa Afrika kwa vijana wa miaka 17, ni mafanikio ya watanzania wote, TFF isiegemee upande mmoja na kusahau mwi ngine.

Timu zote hizo zinakabiliwa na majukumu makubwa katika soka la Afrika, hivyo ni lazima kuwe na mikakati madhubuti itakayoleta mafanikio kwa Stars kwa kufuzu AFCON, lakini pia kwa Serengeti Boys kutwaa ubingwa wa Afrika kwa vijana wa umri huo.

Moja ya mikakati ni kuhakikisha  Serengeti Boys inapata michezo ya kutosha ya kimataifa ya kujipima nguvu na mataifa yaliyopiga hatua kubwa katika soka.

Kwa kufanywa hivyo italisaidia  benchi la ufundi la timu Serengeti Boys kubaini mapungufu yaliyopo katika kikosi cha timu hiyo na kuyatafutia ufumbuzi mapema kabla ya kuingia mashindanoni.

Jambo la kufurahisha ni kwamba vijana wanaounda kikosi cha Serengeti Boys wameonyesha nia mapema kwamba kuna kitu wanakitaka, hivyo kwa kuwaandalia mazingira  mazuri kabla ya kushiriki michuano ya Afrika hapo mwakani ni wazi kuna jambo kubwa la kupendeza watalifanya kwa Taifa lao la Tanzania.

Mafanikio ya Stars kufuzu AFCON itakuwa ishara pia ya kufuzu  Kombe la Dunia  siku zijazo, pia kwa Serengeti Boys kupata nafasi ya kucheza Kombe la Dunia.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles