26 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

‘Tendeni haki kwa walimu’-Prof. Komba

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Wajumbe wa Kamati za Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) ngazi ya Wilaya wametakiwa kuzingatia maadili na miiko ya utumishi wao katika kutekeleza majukumu yao ili waweze kifikia malengo ya Tume ya kutoa huduma bora kwa haki kwa walimu wote nchini.

Kauli hiyo imetolewa Februari 8, 2021 na Mwenyekiti wa TSC, Prof. Willy Komba, wakati akifungua mafunzo yaliyowahusisha Wajumbe wa Kamati za TSC kutoka Wilaya za Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Morogoro yalinayofanyika mjini Morogoro.

Ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Na. 25 ya mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2016, Kamati za Wilaya zimepewa mamlaka ya kusimamia Maadili na Maendeleo ya walimu, hivyo mamlaka hayo yakitumika vibaya haki haiwezi kutendeka kwa walimu.

“Kamati za Wilaya zimepewa nguvu kubwa kisheria katika kuamua masuala ya ajira, maadili na maendeleo ya walimu, hivyo kitu kikubwa mnachopaswa kuzingatia ni maadili ya utumishi wenu ili muweze kutenda haki kwa walimu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinazohusika,” amesema Prof. Komba.

Mwenyekiti wa TSC, Pro. Willy Komba (katikati kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Makamishana wa Tume (Waliokaa) pamoja na baadhi ya wajumbe wa mafunzo ya Kamati za Wilaya yaliyofanyika mkoani morogoro.  Kushoto kwa Mwenyekiti ni Kaimu Katibu wa Tume, Moses Chitama na wa kwanza upande wa kulia (aliyekaa) ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu, Robert Lwikolela

Prof. Komba ameeleza kuwa Tume hiyo imebaini changamoto kadhaa za kiutendaji katika Kamati za Wilaya kitu kinachosababisha baadhi ya walimu kunyimwa haki zao za msingi hususan wakati wa kushughulikia mashauri ya nidhamu ya walimu.

“Tukiwa tunashughulikia rufaa za walimu, tumeona kuwa miongoni mwa hoja nyingi za warufani ni Mamlaka za Nidhamu (Kamati za Wilaya) kutozingatia taratibu za uendeshaji wa mashauri zilizowekwa kwa mujibu wa sheria kitu ambacho tumeona kinakwamisha malengo ya Tume katika kutoa huduma bora kwa walimu,” amesema Prof. Komba.

Amesema baada ya kuiona changamoto hiyo, Tume imeanza kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati za Wilaya ili wawe na uelewa wa kutosha wa sheria, kanuni na taratibu za utendaji wao na kuhakikisha kuwa kila mwalimu anahudumiwa kwa haki na kwa wakati.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo ameitahadharisha Kamati hizo kuwa suala la uelewa wa sheria ni jambo moja na utekelezaji wa sheria ni jambo jingine.

Amefafanua kuwa wajumbe wasipokuwa waadilifu wanaweza kukiuka taratibu makusudi ili kutimiza matakwa yao bila kujali maumivu ya walimu yanayosababishwa na kunyimwa haki zao.

“Tunawapa mafunzo kwasababu ni wajibu wa Tume kuwajengea uwezo ili muweze kutekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia sheria. Hata hivyo, mnaweza kuwa na uelewa wa kutosha lakini msipokuwa waadilifu bado hamtawatendea haki walimu. Ninawasihi, kila mmoja azingatie maadili ya kazi yake ili Serikali iweze kufikia azma yake ya kuwahudumia walimu kwa haki,” amesema Prof. Komba.

Naye, Kaimu Katibu wa TSC, Moses Chitama, ameeleza kuwa Kamati za Wilaya zina wajibu wa kuwaelimisha walimu kuhusu haki na wajibu wa kazi yao na siyo kukaa na kusubiri walimu wakosee ili wawachukulie hatua za kinidhamu.

Aliongeza kuwa lengo kubwa la kuanzishwa kwa TSC ni kurahisisha kuduma kwa walimu ili waweze kufundisha wanafunzi kwa ufanisi. Hivyo, ni wajibu wa kila mjumbe kuelewa kuwa Tume inawajibu wa kuwalea walimu ili wasijiingize katika ukiukaji wa maadili na kijikuta wanaadhibiwa.

“Ninapenda tuwe na uelewa wa pamoja kuwa Tume haipo kwa ajili ya kuwafukuza walimu tu. Wapo wajumbe wa Kamati tangu wanachaguliwa hadi wanamaliza muda wao hawajawahi kuwatembelea walimu na kuwaelimisha kuhusu wajibu na haki zao. Ni jambo baya sana endapo huko wilayani unakaa tu kusubiri uletezwe shauri la mwalimu ili umfukuze kazi,” amesema Chitama.

Kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu, Kamati za Wilaya ni Mamlaka ya Nidhamu kwa walimu na miongoni mwa majukumu yao ni kushughulikia masuala ya ajira na maendeleo ya walimu ikiwemo kumpandisha cheo/daraja mwalimu, kumbadilishia muundo wa kazi mwalimu aliyejiendeleza kimasomo pamoja na masuala ya kusimamia nidhamu na maadili ya walimu.

Mafunzo hayo yanahudhuriwa pia na wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Walimu ambao pamoja na majukumu mengine kwa mujibu wa sheria, wamepewa mamlaka ya kuamua rufaa za walimu wanaopinga uamuzi uliotolewa na Kamati za Wilaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles