23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

“Tembeleeni Hifadhi za Taifa kukuza utalii wa ndani”

Na Samwel Mwanga, Serengeti

Watanzania wametakiwa kutembelea hifadhi za Taifa zenye wanyama mbalimbali  zilizopo hapa nchini ili kukuza utalii wa ndani na kuondoa dhana kuwa utalii huo ni kwa ajili ya wageni kutoka nje ya nchi hasa nchi za Ulaya.

Wafanyakazi wa Mauwasa wakiangalia Mamba na Viboko(hawapo pichani)katika hifadhi ya mbuga ya Wanyama ya serengeti mkoani Mara.

Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Mtembeza Watalii ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Vicent Paschal wakati akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa(Mauwasa) iliyoko wilaya ya Maswa  mkoa wa Simiyu waliotembelea hifadhi hiyo.

Amesema Watanzania walio wengi wanashindwa kutembelea mbuga za wanyama ambazo ni vivutio vikubwa katika nchi yetu huku wakidhani kuwa utalii ni kwa ajili ya wazungu tu.

Amesema licha ya Tanzania kuwa na utajiri mkubwa wa raslimali ikiwemo mbuga za wanyama na maajabu mengine kama kuwepo kwa Twiga weupe ndani ya nchi hii ambapo Watanzania wamekuwa wakistaajabu pindi wanapo tembelea maeneo hayo ambayo hata gharama zake za kitalii ni ndogo kwa wazalendo ikilinganishwa na watalii wa kutoka nje.

Amesema baadhi wamekuwa wakistaajabu kuona mali asili hizo katika chaneli za luninga kutoka nje lakini kumbe wanyama, ndege na wadudu na maajabu mengine yapo hapa hapa nchini.

Simba wakiwa katika mbuga ya Wanyama ya Serengeti mkoani Mara(picha na Samwel Mwanga).

“Jamani maliasili zingine ziko kando kando tu mwa vijiji vyenu lakini mmekuwa mkiwashangaa wanyama hao kwenye luninga licha ya kuwepo kwa gharama ndogo za kitalii kwa Mtanzania,” amesema.

Amesema inashagaza kuona watanzania kuwa na utamaduni wa kusimuliwa jambo badala ya kwenda kujionea mwenyewe kwa macho ndani ya nchi yako kwa gharama nafuu na wao kuwa mabalozi wazuri popote wanapo kwenda.

Queen Mlangala ambaye ni Mtumishi wa Mauwasa licha ya kuipongeza Bodi ya Mamlaka kuwawezesha kutembelea mbuga hiyo pia wamejionea wanyama mbalimbali ambao mara nyingi wamekuwa wakiwaona kupitia runinga.

“Tumeona wanyama mbalimbali ndani ya mbuga ya Serengeti wengi wao tulikuwa tukiwaona kupitia runinga kwa kweli bodi yetu ya Mauwasa  imefanya jambo jema sana kutuwezesha kufika katika hifadhi hii ya wanyama,”amesema.

Naye, Leonald Mnyeti akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa amesema wamefanya ziara hiyo ya utalii ili kuwapatia motisha wafanyakazi hao kutokana na kufanya kazi vizuri sambamba na kuunga mkono Royal Tour iliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu kuzitembelea na kuzitangaza Mbuga zetu za Wanyama na vivutio vingine vilivyopo hapa nchini.

Amesema ni vizuri taasisi nyingine za serikali na mashirika ya watu binafsi kuwapatia ruhusa wafanyakazi wao ili wawezs kutembelea mbuga za wanyama na vivutio vingine vilivyoko hapa nchini ili kuweza kuunga juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan uvitangaza vivutio vyetu tulivyonavyo.

“Nitoe wito kwa taasisi za serikali na zile binafsi ziwawezeshe watumishi wake watembelee vivutio mbalimbali vilivyoko  hapa nchini na hii tutamsaidia Rais wetu Samia Suluhu katika jitihada zake za kuvitangaza vivutio vyetu,”amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles