Na ANDREW MSECHU – Dar es Salaam
VITUO vya televisheni vya ndani vimepewa mwezi mmoja kulipia ada za urushaji wa matangazo yao katika ving’amuzi vyenye kibali, vinginevyo vitaondolewa.
Agizo hilo lilitolewa jana na umoja wa waendeshaji wa ving’amuzi vya Ting, Continental na Star Times, ambavyo ndivyo vyenye kibali cha kurusha bure chaneli hizo.
Agizo hilo linakuja siku chache baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuagiza ving’amuzi vya DSTV, Azam na Zuku, kuondoa chaneli hizo za ndani kwa madai kuwa hawana leseni ya kuzirusha.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa umoja huo, Mchungaji Dk. Vernon Fernandez, alisema kwa miaka 10 sasa wamepata hasara kutokana na vituo hivyo vya televisheni kutolipa ada wanayopaswa kulipa kwa mujibu wa sheria.
“Tunatoa muda wa mwezi mmoja, ambaye hatolipia ada za urushaji wa matangazo, atakatiwa huduma mara moja. Lakini tunatoa pia nafasi ya wale wanaoona ipo haja ya kuzungumza waje, kwa sababu suala hili lina gharama za malipo ambazo wanatakiwa kuingia,” alisema.
Alieleza kuwa malipo hayo yanafikia Sh milioni 2.4 kwa mwezi kwa kila sehemu yenye mnara kulingana na mahitaji ya wahusika kufikia watazamani wengi zaidi.
Dk. Fernandez alisema kwa sasa umoja huo una minara inayofikia 47 katika mikoa 26 nchini, lakini wamejikuta wakipata hasara katika kipindi chote cha miaka 10 sasa kutokana na kurusha bure matangazo ya vituo vya televisheni za ndani.
Fernandez alisema hasara waliyoipata kwa muda wote huo, inatokana na ving’amuzi vya kulipia kubeba chaneli za bure (FTA) suala lililoathiri mauzo ya ving’amuzi na kupungua kwa malipo ya kila mwezi.