29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

TEKNOLOJIA SASA KUTUMIKA KUKABILI ATHARI ZA TUMBAKU

Na VERONICA ROMWALD, ALIYEKUWA KENYA

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa zaidi ya watu bilioni moja duniani wanavuta sigara, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo 2025.

Kila mwaka shirika hilo linakadiria takriban watu milioni saba hufariki dunia kutokana na matumizi ya bidhaa hiyo inayotokana na zao la tumbaku.

Linaonya idadi ya vifo na wavutaji itaongezeka ikiwa juhudi hazitachukuliwa kuisaidia jamii kupunguza ama kuachana kabisa na matumizi ya bidhaa hizo.

Katika kuhakikisha Dunia inafikia lengo la kupunguza kama si kuondoa kabisa matumizi ya bidhaa hiyo, wadau muhimu hasa katika sekta ya tumbaku walikutana hivi karibuni huko Naivasha nchini Kenya.

Wadau hao walijadiliana jinsi ya kufikia lengo hilo katika warsha hiyo ya siku mbili hasa jinsi ambavyo mbinu ya teknolojia mpya itakayoweza kusaidia kupunguza madhara ya tumbaku ili kukomesha kabisa uvutaji sigara.

Katika warsha hiyo iliyoangaliwa na Kampuni ya Oxegene nchini humo ilipewa kauli mbiu: “Kupunguza madhara ya tumbaku, kuelekea ulimwengu usio na moshi.”

Waandishi wa habari kutoka Tanzania, Nigeria, Botswana, Ethiopia na Kenya, nchini Malawi, Lesotho, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Swaziland, Uganda, Afrika Kusini, Zambia, na Zimbabwe walishiriki katika mjadala huo.

Ade Adeyami ambaye ni Rais wa Taasisi ya Leadership Impact Dynamics ni miongoni mwa watoa mada wakuu waliohudhuria.

Anasema juhudi zinahitajika kukabiliana na jambo hilo na kwamba ikiwa hazitafanyika itakuwa vigumu kufikia lengo namba tatu la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

“Lengo namba tatu la SDGs linasisitiza kuhusu afya bora kwa wote, lakini idadi ya wavutaji ni kubwa tena tafiti zinaonesha kiwango ni kikubwa zaidi barani Afrika ikilinganishwa na mabara mengine duniani,” anasema.

Anasema kutokana na hali hiyo ni muhimu kukubaliana  na mbinu hasa za kiteknolojia na za kibunifu zitakazosaidia kupunguza idadi ya wavutaji barani humo.

Magesha Ngwiri ambaye anajihusisha na masuala ya Ushauri kwa Vyombo vya Habari anasema kuna umuhimu kwa wanahabari barani humo kujikita katika kufanya tafiti za kina juu ya athari za matumizi ya bidhaa zitokanazo na tumbaku.

“Takwimu za WHO zinaonesha Bara la Afrika linaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha matumizi ya bidhaa hizo kwa kiwango cha asilimia 80 ikilinganishwa na mabara mengine, ni kiwango cha juu mno.

“Matokeo ya utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kati ya mwaka 2010 na 2011 vijana wa umri wa kati ya miaka 13 hadi 15 Barani Afrika walionekana kuwa wameanza kutumia bidhaa hizo,” anasema

Anaongeza: “Kama hali ilikuwa hivyo unaweza kutafakari tupo wapi sasa na tunaelekea wapi, jamii inahitaji kupatiwa elimu ya kutosha kuhusu athari zitokanazo na matumizi ya bidhaa hizo.

“Hivyo, ni wazi kwa kufanya tafiti za kina kutasaidia kuipatia elimu ya kutosha jamii juu ya athari zitokanazo na bidhaa hizo na kuziamsha serikali kuchukua hatua kukabiliana na jambo hilo ili kuokoa kizazi cha Afrika,” anasema.

Mhadhiri na Mwanachama wa Kudumu wa Taasisi ya Biashara ya Gordon – Chuo Kikuu cha Pretoria, Dk. Tendai Kadenhe Mhizha anasema kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) zilizotolewa mwaka 2012 vilitokea takriban vifo milioni 38 duniani.

“Asilimia 68 ya vifo hivyo vilitokana na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza, ambavyo huchangiwa pia na matumizi ya bidhaa hizo,” anasema.

Anasema jamii inategemea kuona wafanyabiashara waliopo katika sekta ya viwanda na uzalishaji wa tumbaku wanahusika moja kwa moja katika kuzuia matumizi ya bidhaa hiyo.

“Kampuni na wadau waliopo kwenye sekta hii wanajua kuna mamilioni ya wanaume na wanawake wanaotumia bidhaa zao lakini wawajibike kuhakikisha dunia inafikia lengo lake la kuwa na jamii isiyovuta moshi katika siku zijazo,” anasema.

Anasema kuja na teknolojia mpya ikiwamo ya E-Cigarettes kutasaidia kupunguza madhara yanayosababishwa na sigara ambazo hutengenezwa kwa malighali ya zao la tumbaku.

Katika mkutano huo uliundwa Mtandao wa Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Waandishi wa Habari wanaopigania jitihada za kupunguza madhara ya tumbaku.

Barnaba Thondhlana ambaye ni mwandishi wa habari wa kujitegemea kutoka nchini Zimbambwe anayefanya kazi na Jarida la ‘Independent in South and African Leadreship’ la nchini Uingereza aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa mtandao huo.

Mshauri wa ‘Digital Media’ nchini Kenya, David Ohito aliteuliwa kuwa Mratibu wa mtandao huo ambapo wadau hao walikubaliana pia kwamba ipo haja ya kufanyika uwekezaji mkubwa katika bidhaa mbadala zitakazosaidia wavutaji sigara kupunguza hatari ya kupata madhara yatokanayo na sigara.

Aidha, waandishi walikubaliana kujikita zaidi katika kuandika habari za afya zitakazoelimisha jamii hususan vijana ‘kutojiingiza’ katika uvutaji sigara.

Walishauri makampuni ya sigara kuanza kufikiria kutumia mbinu mbadala ya kiteknolojia itakayosaidia kupunguza madhara yatokanayo na bidhaa hiyo ili kuokoa afya za watumiaji na jamii kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles