24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Teknolojia mpya yatambulishwa kukabili vifo vya mama na mtoto

Na Yohana Paul, Mwanza

Katika juhudi za kupunguza vifo vya mama na Mtoto taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Kamanga Health Care Foundation (KHF) imetambulisha rasmi matumizi ya teknolojia inayofahamika kama Non-Stress Test (NST) kwa kina mama wajawazito ili kufuatilia mwenendo wa mtoto tumboni.

Akizungumzia teknolojia ya NST, Mwenyekiti wa Taasisi ya KHF, Dk. Mercy Minde amesema utambulisho wa teknolojia hiyo itakayoanza kutumika Januari 2021 unaenda sambamba na kuzinduliwa rasmi kwa taasisi hiyo ambayo inalenga kusaidia serikali kutoa huduma za afya kwa gharama nafuu na kwa wakati kwa makundi maalumu.

Dk. Minde amesema miongoni mwa makundi ambayo taasisi hiyo imeyalenga ni kundi la kina mama wajawazito ambapo matumizi ya teknolojia ya NST itawasaidia kutambua mapigo ya moyo ya mtoto tumboni na hivyo kumpatia mama tahadhari na huduma kulingana na mabadiliko yatakayobainika ili kukabili changamoto zinazoweza kumfanya mama ama mtoto kupoteza maisha.

Amesema makundi mengine waliyoyalenga kuyafikishia huduma bora za afya kwa wakati na kwa gharama nafuu ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu, watoto yatima na wale wenye uhitaji wa huduma ya afya ya haraka hasa majeruhi wa ajali wasiokuwa uwezo wa kugharamia matibabu na vipimo vya awali.

Dk. Minde ambaye pia ni Daktari Bingwa wa watoto amesema mbali na huduma ya afya ya mama na mtoto, pia Taasisi hiyo imedhamiria kujikita katika kutoa mafunzo kwa wauguzi, kusaidia huduma za upasuaji, huduma za kinywa na meno na huduma za uchunguzi na tiba kwa gharama nafuu.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk. Fabian Masaga aliipongeza taasisi hiyo kwa kuja na matumizi ya  NST kwani afya ya mama na mtoto ni eneo nyeti na kuwaomba watoa huduma za afya wote kutoka taasisi binafsi na zile za serikali kuwajibika kikamirifu kuisaidia serikali kufikia adhima ya kumaliza vifo vya watoto wachanga.

Awali, akizindua rasmi taasisi ya KHF kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Kaimu Mgeni Rasmi ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Pius Rutachunzibwa amesema matumizi ya teknolojia ya kisasa kwenye sekta ya afya ndiyo jambo linalohitajika kwa sasa hivyo ni vyema hospitali zingine mkoani hapa zitafute namna ya kuanza kutumia NST ili kukabiliana na vifo vya watoto wachanga.

Dk. Rutachunzibwa amesema uzinduzi wa taasisi ya KHF inayofanya kazi chini ya Kamanga Hospital ni maendeleo makubwa kwa hopitali hiyo ya rufaa ya kanda kwani itasaidia kuboresha huduma za afya na kuwezesha makundi tofauti kupata huduma kwa gharama nafuu na kusaidia kufanikisha sera ya serikali ya huduma bora za afya kwa kila Mtanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles