Na Albert Mkongwa
TAFITI mbalimbali zimeonyesha kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi katika Bara la Afrika yenye idadi kubwa ya matumizi ya simu za mkononi kwa wananchi wake, kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ikumbukwe kuwa tafiti za hivi karibuni zimeonyesha kuwa ni asilimia 11 tu ya Watanzania walio watu wazima ambao wana akaunti katika benki na taasisi za fedha. Hii inaonyesha kuwa bado matumizi ya huduma za kibenki yapo chini sana katika nchi yetu.
Pamoja na kuwa Tanzania ina zaidi ya benki 50 yaliyosajiliwa na baadhi ya benki hizo tayari zinatoa huduma za kibenki kupitia simu za mikononi (Mobile Banking services), bado inaonyesha wazi kuwa matumizi ya teknolojia hii ya mawasiliano ya simu za mkononi inaweza kutumika kwa ufanisi zaidi na mabenki katika kuongeza wigo wa huduma za kibenki kuwafikia wale ambao bado hawajafikiwa na huduma zakibenki (Financially excluded).
Matumizi ya teknolojia hii ya simu za mkononi katika kutoa huduma za kibenki yanaweza kutoa mchango mkubwa zaidi hasa kwa kutoa huduma kwa maeneo yaliyo vijijini na kwenye miji midogo ambako hakuna kabisa huduma za kibenki.
Ikumbukwe kuwa mara kwa mara Serikali imekuwa ikisisitizia benki na taasisi nyingine za fedha kupanua huduma zao na kuwekeza nje ya miji mikubwa na kuelekeza huduma zao katika maeneo ya vijijini na miji midogo ili kukuza uchumi wa maeneo hayo. Hii ni kutokana na kwamba benki nyingi hazina matawi katika maeneo ya vijijini na hivyo kushindwa kutoa huduma hizo katika maeneo hayo.
Huduma hii ya kubenki kwa kutumia simu za mikononi imekuwa ikipata umaarufu kwa idadi kubwa zaidi ya benki kuanza kutoa huduma hii, ambapo hapo awali hayakuwa yanatoa. Mategemeo ni kuwa mabenki mengi zaidi yataendelea kuongeza huduma hii katika orodha ya huduma wanazozitoa kwa wateja wao, kutokana na umuhimu wake katika kuongeza idadi ya wateja wa benki husika na pia kuweza kujipatia mapato zaidi na kutumia fursa ya kukua kwa teknolojia ya mawasiliano na hasa simu za mkononi.
Huduma za kibenki zinazoweza kupatikana kwa simu ya kisasa ya mkononi (Mobile Banking)
Zipo huduma mbalimbali ambazo zinaweza kupatikana kwa kutumia simu za mkononi, zikiwemo hizi zifuatazo:
- Kupata salio katika akaunti ya mteja.
- Kutuma /kuhamisha au kupokea fedha kwa akaunti ya mteja wa ndani na nje ya benki husika.
- Kupata taarifa ya fedha (Bank Statement).
- Kupata taarifa mbalimbali za fedha za kigeni na taarifa nyinginezo nyingi kuhusiana na mambo ya fedha.
- Kulipia huduma mbalimbali mtandaoni.
Faida za kutumia huduma za kibenki kwa kutumia simu ya mkononi
- Huduma hii inaweza kupatikana mahali popote na wakati wowote (Masaa 24) tofauti na huduma ambazo ni lazima mteja afike katika tawi la benki husika ambapo kuna muda wa kufungua na kufunga benki
- Huduma hizi hazina gharama na kama kuna gharama basi gharama zake ni ndogo
- Kwa kutumia simu ya mkononi, mteja anaweza kufanya miamala mbalimbali kama ilivyoainishwa hapo juu kuhusu huduma zinazoweza kupatikana kwa kutumia simu za mkononi
- Huduma hii ni salama zaidi ukilinganisha na huduma za kibenki kwa mtandao (On line Banking)
Changamoto
Pamoja na kukua kwa matumizi ya teknolojia ya simu za mkononi katika kutoa huduma za kibenki, eneo hilo lina changamoto mbalimbali zikiwemo hizi zifuatazo:
- Usalama (Security) wa huduma kwa maana ya uwezekano wa wizi wa kimtandao kutokea
- Si simu za aina zote ambazo zinaweza kutumika katika kumwezesha mteja kupata huduma za kibenki. Ni simu za kisasa tu (Smart phones) au ‘simu janja’ ndio zenye uwezo wa kutumika kutoa huduma hizi.
- Huduma hizi zinaweza kupatikana tu pale mawasiliano ya simu (network) yanapokuwa hewani (on line).
- Katika mazingira mengine ni lazima mtumiaji wa simu za kisasa (Smart phone) aweze kupakua (download) application au program ambayo itamwezesha kupata huduma hizi.
- Simu ya mkononi ikiibiwa, ni rahisi kwa taarifa za fedha kutumiwa na mtu mwingine na hivyo kusababisha upotevu wa fedha na taarifa.
Nafasi za benki katika kuongeza matumizi ya huduma hii
Kutokana na maendeleo katika teknolojia ya simu za mkononi, benki na taasisi za fedha zinaweza kufanya yafuatayo:
- Kutoa elimu zaidi kwa wateja wao na pia watumiaji wengine wa simu za mkononi waliopo maeneo ya vijijini na hata mijini kuhusu manufaa ya kutumia simu za mkononi ili kuwawezesha kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki mahali popote na wakati wowote.
- Kwa kushirikiana na makampuni ya simu za mkononi kama vile Vodacom, Tigo, Airtel n.k. kuhakikisha kuwa mitandao ya simu inafika katika maeneo mengi zaidi ya vijijini na miji midogo nchini ili huduma hizi za kibenki ziweze kupanuliwa zaidi.
- Kuimarisha mifumo ya usalama katika mitandao ya simu kwa kushirikiana na wataalamu wa teknolojia ya kompyuta ili kuondoa hofu na wasiwasi kuwa matumizi ya huduma hizo ni salama na taarifa na fedha zao zitaendelea kuwa salama kwa wakati wote.
Ni matumaini yangu kuwa benki na taasisi nyingine za fedha zitajikita zaidi katika kuangalia fursa hizi na kuwekeza zaidi katika eneo hili la huduma za kibenki kwa kutumia teknolojia ya simu za mkononi katika kupanua wigo wa watumiaji wa huduma za kibenki nchini ili kuongeza mchango wa sekta ya fedha katika ukuaji wa uchumi nchini kwa kutoa huduma jumuishi na kuongeza mchango wake katika kiwango chake katika pato la Taifa (GDP) ambacho bado ni cha chini sana.
(Mwandishi Albert E Mkongwa ni Mtaalamu Mbobezi katika maswala ya Kibenki na Fedha na ni mwanachama wa TIOB).