27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

SHONZA: TAMASHA LA UTALII KUINUA UTALII WA NDANI 

 

NA OCTAVIAN KIMARIO-WHUSM


 

KUTOKANA na tafiti mbalimbali zilizofanyika Tanzania, utalii ni sekta ambayo ina nguvu ya uzalendo, amani na utajiri ambao ni zawadi na karama kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kuijalia nchi ya Tanzania kuwa na neema ya vivutio vingi vya utalii tofauti na nchi nyingine ulimwenguni.

Tanzania ni ya pili kwa vivutio duniani baada ya Brazil.

Hivyo, kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, Taasisi ya Mtandao wa Wasanii wa Musiki wa Injili nchini, Tanzania Gospel Artists Network (Tagoane) imehamasika kuwa na wazo la mradi  katika kutangaza  vivutio mbalimbali vya utalii, utamaduni wa Mtanzania na kuhamasisha utalii wa ndani kuanzia ngazi ya kaya hadi kwenye wakala wengine wa malezi ikiwemo shuleni, vyuoni.

Tanzania Gospel Artists Network (Tagoane) ni mtandao wa wasanii wa tasnia ya Injili Tanzania uliosajiliwa na Serikali wenye dhamira ya kuwaleta wasanii wa tasnia ya Injili pamoja ili kufikia malengo yaliyotarajiwa kwa mujibu wa dira na maono elekezi kulingana na katiba yao.

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, amezindua Tamasha la Utalii lililopewa jina la ‘Tanzania Tukuza Utalii Festival Genesis 1’ lililoratibiwa na Tagoane likiwa na lengo la kukuza utalii wa ndani nchini.

Katika uzinduzi wa tamasha hilo, Shonza ametoa wito kwa wasanii wengine na wadau mbalimbali kuiga mfano wa Tagoane katika juhudi za kuutangaza utalii wa ndani nchini.

“Niwaombe wadau wa sanaa na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii muige juhudi hizi zilizooneshwa na Tagoane ili kuhamasisha Watanzania kupenda kutembelea vivutio vyetu vya utalii,” anasisitiza Juliana.

Aidha, Naibu Waziri amesema Serikali itaendelea kuwaunga mkono na kufanya kazi bega kwa bega na wadau mbalimbali watakaojitokeza kutangaza utalii nchini.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amesisitiza wananchi kushirikiana na Rais Dk. John Magufuli kutunza amani iliyopo kwani amani  ndiyo kichocheo kikuu katika kuvutia watalii nchini.

“Vijana hatuna budi kudumisha amani na uzalendo kwani tunajua wazi kuwa msingi mkuu wa utalii ni amani, nchi isiyokuwa na amani haiwezi kupata watalii, hiyo ndiyo sababu Tanzania tumekuwa tukipata watalii wengi kutoka katika nchi mbalimbali duniani kutokana na utulivu na amani tuliyonayo,” anaongeza Naibu Waziri.

Akizungumzia matarajio ya mradi huo, Rais wa Tagoane, Dk. Godwin Maimu, anasema mradi unalenga  kumsifu na kumtukuza Mungu kwa njia ya sanaa na tamaduni za Kitanzania kwa kuelimisha jamii pana ya Kitanzania kudumisha na kuendeleza maadili mema na uzalendo kwa vizazi vyote kwa kutekeleza kwa vitendo dhana njema na falsafa ya Uzalendo Mbele, Tanzania Kwanza.

“Kutangaza na kuhamasisha utalii wa ndani kupitia vivutio vya Taifa (Maliasili na Utalii), kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili na kuibua vipaji kwa wasanii wachanga ambao wanaojishughulisha na sanaa hususani wanamuziki binafsi, vikundi (Kwaya na bendi), watayarishaji (Producers), madansa (Dancers), waigizaji ( Actors), waongozaji (Directors) waandishi wa muswada na maandiko,” anafafanua Dk. Godwin Maimu.

Aidha, Dk. Godwin Maimu anaongeza kuwa tamasha hilo linalenga kukuza na kuinua uchumi wa nchi na watu wake kupitia fursa mbalimbali zilizopo kupitia sanaa, maliasili, vivutio vya Taifa na kutangaza umuhimu wa amani na rasilimali hii adimu ya vivutio mbalimbali vya utalii na kuonesha kwa vitendo uzalendo kwa rasilimali tulizojaliwa hapa nchini.

Mbali na hayo, Dk. Godwin Maimu anasema katika kufanikisha Tanzania Tukuza Utalii Festival (TATUFE), inategemea kuwa na matukio mbalimbali ikiwemo kuendesha warsha, semina, makongamano na mafunzo ya umuhimu wa utalii wa ndani kwa umma hususani makundi maalumu kama wanafunzi (shule za msingi, sekondari na vyuo), vijana na wasanii kwa ujumla.

“Vilevile tunatarajia kuandaa makala na filamu (short film) zenye maudhui yenye mlengo wa kuhamasisha uzalendo, maadili, kukuza lugha ya Kiswahili na utofauti wa mwonekano wa vivutio mbalimbali vya utalii,” ameongeza Dk. Godwin Maimu.

Katika kusisitiza malengo ya tamasha hili, Naibu Waziri Shonza mara baada ya ufunguzi wa tamasha, alitembelea hifadhi ya Taifa ya Arusha (Arusha national Park) akiambatana na wasanii, wanafunzi wa shule za msingi na wadau mbalimbali wa utalii mkoani Arusha.

Kaulimbiu ya Tagoane ambayo ni ‘Sauti Moja, Lugha Moja, Tujikwamue Kiuchumi Sanaa ni Kazi’ ambayo dhamira kuu kwa wanachama wake ni kutambua thamani ya vipaji vyao na dhamira ya kuendesha mradi kwa kushirikiana na wasanii na wadau mbalimbali wa sanaa na utalii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles