Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC), limelaani vitendo vya mauaji vinayojitokeza wilayani Mkuranga, Kibiti na Rufiji pamoja na shambulio la kupigwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu Septemba 7, mwaka huu mjini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais Baraza hilo, Askofu Beatus Kinyaiya matendo hayo yanalifedhehesha taifa.
Amesema maaskofu wa katoliki wanatoa pole kwa wote waliofikwa na matatizo hayo na kuwaombea wale waliopata matatizo mbalimbali.
“Matendo kama haya ni dhambi, si uhalifu wala si utamaduni wa Watanzania, Mwenyezi Mungu awaponye waliopata matatizo na kuwarehemu waliofariki.
“Baraza linatamani kuona wale wote waliokua nyuma ya matendo hayo ya utesaji, utekaji, wauaji, wanatafutwa na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema Askofu Kinyaiya katika taarifa yake hiyo.