Na Esther Mnyika,Mtanzania Digital
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema elimu kuhusu usalama wa mtandao inahitajika ili kudhibiti uhalifu wa mtandao.
Hayo yamebainishwa leo Februari 2, 2024 jijini Dar es Salaam na MkurugenzMkuu TCRA, Dk. Jabir Bakari wakati akifungua semina ya wadau wa masuala ya mtandao wa intaneti katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Usalama Mtandaoni .
Amesema kuna haja ya kuwadhibiti wanaotumia mitandao vibaya kwa kufanya matukio ya utapeli kuiba taarifa binafsi za watumiaji wengine kwa lengo la kujinufaisha wenyewe na kuleta matatizo kwa wengine.
“Pamoja na faida za mitandao bado ipo haja kwa wahalifu wa mtandao kudhibitiwa na kupewa elimu ya kutoka kwenye kundi hili la uhalifu na kuwaelimisha wengine kuhusu usalama wa mitandao.
“Pamoja na faida nyingi zitokanazo na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) bado tunaowajibu wa kuendelea kuelimishana kwani kuna baadhi ya watumiaji wanatumia fursa hiyo vibaya kwa kufanya uhalifu, hivyo tunawajibu wa kuwadhibiti,”amesema Dk. Bakari.
Amesema kwa mujibu wa taarifa ya robo ya mwaka hadi Desemba mwaka jana imeonesha kuwa watumiaji wa intaneti Tanzania wamefikia milioni 35.8 huku idadi za simu janja zenye uwezo wa kutumia intaneti ni millioni 19.8.
“Dhana za maendeleo ya teknolojia ya kidigiti kila mmoja ananafasi muhimu ya kuhakikisha anga la mtandao ni salama kwa kuzingatia matumizi sahihi na salama na kuleta tija kwa kila mtu, binafsi pamoja na jamii,”ameongeza.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki katika semina hiyo Dk. Macca Abdalla ambaye ni mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Madirisha Women Cooperative Sector amesema mtandao umemrahisishia matumizi mbalimbali ya teknolojia
Amesema bado baadhi ya wanawake wanaohitaji kupata elimu zaidi ya mtandao ili waweze kujikwamua kiuchumi.