Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imevipiga faini ya mamilioni ya shilingi vituo vitano vya runinga kwa kurusha taarifa ambazo zinakinzana na kanuni za utangazaji kwa kurusha habari ambayo inasadikiwa kuwa na viashiria vya uchochezi.
Vituo vilivyokumbwa na adhabu hiyo ni ITV, EATV, Channel Ten, Azam Two na Star tv.
Akitangaza uamuzi huo Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Joseph Mapunda, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuvihoji vituo hivyo na kukiri kuwa vimetenda makosa hayo.
Akisoma uamuzi wa kamati hiyo, Mapunda alisema kuwa habari zilizoripotiwa na vituo hivyo Desemba 6, mwaka jana, hazikuwa na upande wa pili na hivyo kukosa sifa kimaadili na zingeweza kuhatarisha usalama wa taifa.
Alisema vituo hivyo vinaruhusiwa kukata rufaa katika Tume ya Ushindani Kibiashara kama havikuridhishwa na hukumu iliyotolewa na TCRA.
“Katika adhabu, TCRA imekitoza faini ya shilingi milioni 7.5 Kituo cha Televisheni cha Star kwa kukiuka kanuni za utangazaji,” alisema.
Mapunda alisema kituo hicho kilitangaza habari ambazo hazikuthibitishwa za uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika Novemba 2017.
Alisema kituo hicho kilitangaza habari kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuwa kwenye uchaguzi huo watu walipigwa bila uthibitisho kutoka Polisi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kwa upande wa Kituo cha Televisheni cha Azam Two, mamlaka hiyo pia imekitoza faini ya Sh milioni 7.5 kwa kutangaza uchochezi.
Kituo hicho kimetozwa faini kwa kutangaza taarifa za uchaguzi mdogo wa udiwani wa Novemba 2007 bila kupata upande wa pili wa NEC na Polisi.
Shauri kuhusu Kituo cha Televisheni cha East Africa, Mapunda alisema kamati imekitia hatiani kwa kudaiwa kukiuka kanuni za huduma za utangazaji na kutozwa faini ya Sh milioni 15.
“Shauri kuhusu Kituo Utangazaji cha Channel Ten, kinatuhumiwa kurusha taarifa inayokiuka kanuni za utangazaji kwa kurusha habari ya tathmini ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.
“Kamati iitoza Sh milioni 15 kwa makosa ya kutozingatia mizania. Na kwa kituo cha ITV kinatuhumiwa kurusha habari za uchochezi kilichorushwa Novemba 30, mwaka jana kwa habari za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuhusu tathmini ya uchaguzi mdogo, nao wanatozwa faini ya Sh milioni 15 kwa makosa yote matatu,” alisema Mapunda.