Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya TBL Group imeeleza dhamira yake ya kuendelea kutoa ajira kwa watu wenye ulemavu ikiwamo kuwajengea mazingira rafiki sehemu za kazi badala ya kuwabagua na kuwafanya wakose kujiamini na kujiona si sehemu ya jamii.
Mkakati huo umeelezwa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa TBL Group, David Magesse, alipokuwa anaeleza sababu za kuanzishwa kwa mkakati huo.
Alisema kampuni inao mtazamo wa kutoa ajira bila ya ubaguzi wa rangi, jinsia na ulemavu hivyo iko makini kuhakikisha wafanyakazi wake wote inaowapatia ajira wanafanya kazi katika mazingira bora na kupata haki zao zote sawa.
“Kwa upande wa wafanyakazi wenye ulemavu tumewajengea mazingira rafiki ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao vizuri na tumekuwa tukishirikiana na taasisi ya CCBRT ambayo imekuwa ikitupatia miongozo inayotakiwa yakiwamo mafunzo ya ushirikishwaji wao katika majukumu ya kampuni bila kuwaacha nyuma.”
Magesse alisema kampuni imeajiri watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali pamoja na kuwapatia fursa za maamuzi na kutoa mawazo yao kwa kujenga miundombinu rafiki kwao katika kupata huduma zinazostahili.
Magesse alisema kampuni itaendelea kufanya kazi kwa karibu na taasisi ya CCBRT ambayo pia itawasaidia wanapohitaji kutoa ajira kwenye nafasi za watu wenye ulemavu kuwapata wenye sifa zinazostahili kwa nafasi za taaluma mbalimbali zinazokuwepo.
“Kwa ushauri wa wataalamu, kampuni imefikia viwango vya utekelezaji kanuni na miongozo ya kuwajengea watu wenye ulemavu mazingira mazuri sehemu za kazi kwa mujibu wa mwongozo wa Shirika la Kazi Duniani na sheria inayohusiana na huduma kwa watu wenye ulemavu ya mwaka 2010.
Aidha, Magese alisisitiza kuwa katika muda wote ambao kampuni imewapatia ajira watu wenye ulemavu wamegundua kuwa wakijengewa mazingira bora sehemu za kazi wanafanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu na ametoa wito kwa taasisi mbalimbali kuwapatia fursa za kushiriki kutoa mchango wao katika ujenzi wa Taifa.