KOKU DAVID-DAR ES SALAAM
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), imefanikiwa kujenga nyumba 219 kati ya 851 ilizotarajia kujenga kwaajili ya watumishi wa serikali katika eneo la Bunju jijini Dar es Salaam.
Ujenzi wa nyumba hizo ni utekelezaji wa mradi wa nyumba 2500 nchi nzima kila mwaka ambao ndani ya miaka minne TBA imepangwa kujengwa nyumba 10,000.
Akizungumza na Mtanzania jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Kaimu Meneja Usimamizi wa Miliki wa TBA, Fredy Mangula amesema kuwa wamesitisha kwa muda ujenzi wa nyumba kutokana na uhamiaji wa serikali jijini Dodoma ambapo kumeathiri soko la nyumba katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema walitarajia kujenga nyumba 851 maeneo ya Bunju na Gezaulole lakini wamesitisha na badala yake wameelekeza nguvu Dodoma ambako wanatarajia kuanza na ujenzi wa nyumba 100 kwaajili ya watumishi wa serikali.
“Hivi sasa nguvu tunaielekeza Dodoma na tunatarajia kujenga nyumba 100 ambazo tutazijenga katika maeneo ya Nzugumi kwaajili ya watumishi wa serikali lakini wale wa kawaida na katika maeneo ya Itega tutajenga nyumba za viongozi,” amesema Mangula.
Amesema katika nyumba zilizojengwa Bunju, zote wanunuzi wameshahamia na kwamba TBA imesaini mkataba na benki za BOA na NMB kwaajili ya mradi wa nyumba za Bunju ambazo zitakapokamilika watumishi wa serikali watakopeshwa.
Sambamba na Bunju, pia katika kiwanja namba 93/1 Sida Estate TBA imejenga nyumba ya gorofa nane ambayo familia 16 zinaishi ikiwa ni pamoja na sakafu tatu zikiwa zimepangishwa kibiashara.
“TBA tuna wapangaji wa aina mbili ambao ni watumishi wa serikali na wasio wa serikali na wale wa serikali wanalipa kodi 2/3 ya bei ya soko na wasio watumishi wa serikali wanalipa kodi ya itakayokuwa imekadiriwa kulingana na soko,” amesema Mangula.