Matapeli watumia jina la askofu Rwai’chi kuomba fedha

0
618

Aveline Kitomary, Dar es salaam

KATIBU Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki Dar es Salaam, Frank Mtavangu, ametoa tahadhari ya kuwepo kwa ukurasa wa facebook bandia ambao unatumiwa na matapeli kuomba fedha huku wakitumia jina la Askofu Mkuu wa jimbo hilo Yuda Rwai’chi.

Taarifa iliyotolewa na katibu huyo jana jijini Dar es Salaam ilisema matapeli hao wamekuwa wakidai kuwa wanaomba mchango kwaajili ya ujenzi wa makazi ya malezi ya wajane, yatima na wakongwe.

“Napenda kuwatahadharisha kuwa kuna matapeli wamefungua akaunti ya Facebook kwa jina la Askofu Mkuu Yuda Thadei Rwai’chi akaunti hii niya kitapeli inayotumia jina la “Askofu Ruwai Chi”.

“Inaomba watu wachangie ujenzi wa makazi kuu ya malezi ya wajane, yatima na vikongwe ikiomba michango itumwe kwenye (anataja namba ya simu),”alieleza Mtavangu.

Alisema Askofu hatumii akaunti hiyo na hajawahi kuomba michango ya namna hiyo kwa njia hii na akaunti hiyo sio yake .

 “Taarifa juu ya tukio hili imesharipotiwa katika kituo kikuu cha polisi  kati Dar es Salaam.

“Naomba tunapopata wasiwasi juu ya matangazo au maombi yoyote hasa kuhusu masuala ya fedha tuwasiliane na ofisi za jimbo au za parokia zetu na tuwe makini na taarifa za mitandaoni,”alisema Mtavangu.

Taarifa hiyo inakuja ikiwa ni siku chache tangu Askofu Ruwai’chi atokeo katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili (MOI), alikufanyiwa upasuaji mkubwa wa kichwa.

Askofu Ruwai’chi alifanyiwa upasuaji huo baada ya kubainika kuwa anasumbuliwa na tatizo la damu kuvujia ndani ya kichwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here