Na PENDO FUNDISHA – MBEYA
SHIRIKA la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), limetoa mwezi mmoja kwa wananchi na watumishi wake wanaomiliki vifaa mbalimbali vya reli kinyume cha utaratibu, kuvirejesha serikalini kabla ya msako wa nyumba kwa nyumba haujaanza.
Hayo yalielezwa jana na Ofisa wa Polisi Kikosi cha Reli, Jackson Mwakagonda, alipozungumza na watendaji wa vitongoji, vijiji, kata na madiwani wa Halmashauri ya Mbarali na Mbeya.
Alisema miaka kadhaa iliyopita shirika hilo liliyumba katika uchumi hali iliyochangia baadhi ya watumishi ambao si wazalendo kwa kushirikiana na wananchi, kuuza baadhi ya vifaa muhimu vya reli na wengine kuvitumia kwa matumizi ya nyumbani.
“Hapa mnatueleza kwamba wapo watumishi walikuwa wakiuza nondo kwa wananchi.
“Wapo watumishi ambao nao wametumia nondo hizo wengine wanamiliki mataluma na wapo ambao kazi yao ni kuuza vyuma chakavu na spea muhimu za gari moshi.
“Hawa wote hatutawaacha salama, bora wakasalimisha vifaa hivi kabla ya msako wa nyumba kwa nyumba haujaanza,” alisema.
Alisema Serikali imetenga fedha nyingi kuboresha miundombinu ya reli, hivyo kabla ya mchakato huo haujaanza, ni vema wananchi au watumishi ambao walijimilikisha mali za Tazara wakazirejesha.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika, alisema Serikali imetoa Sh bilioni 10 za maboresho ya reli, hivyo haitapenda kuona baadhi ya watu wakiendelea kulikwamisha shirika hilo kwa masilahi yao binafsi.
“Shirika hili liligeuzwa kuwa ni sehemu ya biashara kwa watu kuuza vifaa, wapo wengine walilifanya ni kitega uchumi kwa kuiba vyuma na kwenda kuuza.
“Baadhi wametumia nondo kwenye ujenzi wa nyumba, ni vema wakazirejesha wenyewe, hatua hii haitamwacha mtu salama,” alisema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Igalako, Thomas Mgumba na Mwenyekiti wa Kijiji cha Motomoto, Balensi Mwanjikwa, wamekiri kwamba baadhi ya wananchi wanaoishi kando kando ya reli wamejimilikisha mali hizo, lakini asilimia kubwa walikuwa wakizinunua kutoka kwa watumishi.