28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

TATTOO HUWAATHIRI ZAIDI WAAFRIKA KULIKO WAZUNGU


Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

TATTOO ni uchoraji wa mwili kwa kutumia wino ambao hupenya hadi kwenye ngozi ya ndani na kubadilisha mwonekano wako katika maisha yako yote au kwa muda tu, inateemea na uwekaji.
kwa dunia ya sasa kujichora tatoo imekuwa fasheni.

Michoro hiyo hubeba ujumbe mbalimbali kulingana na matakwa ya mhusika.

Juma Kassim kijana mwenye umri wa miaka 28 mkazi wa Sinza Kijiweni amechora tattoo ya jina la mwenzi wake shingoni mwake.

“Nampenda mpenzi wangu, niliamua kuchora tattoo hii shingoni ili kumuonesha jinsi gani nampenda na namthamini,” anasema.

Kassim anasema hakusudii kuja kuifuta tattoo hiyo kamwe katika maisha yake.

“Ikiwa itatokea nikaachana naye pia siwezi kuifuta hata itokee jambo gani, hii nimeichora itakaa milele katika mwili wangu,” anasema.

Maria Elius anasema yeye amechora tattoo kwa kuandika jina la mama yake.

“Mama yangu amefariki mwaka 2013 nilijihisi mpweke mno, baba yangu simjui, sijawahi kumuona… nilielezwa na mama kwamba alimkimbia nikiwa bado sijazaliwa.

“Hivyo, alinikataa nikiwa tumboni mwa mama, nikaishi bila kumjua baba yangu hadi leo, mama alipofariki nilibaki kwa babu yangu, mwaka 2015 nikaamua kuchora tattoo hii,” anasema.

Anasema kila anapoitazama tattoo hiyo aliyoichora katika mkono wake wa kulia anahisi yupo karibu na mama yake.

“Najua si kweli lakini najihisi vizuri pale ninapomkumbuka naitazama tattoo hii najisikia faraja,” anasema.

Asilimia kubwa ya vijana hujichora tattoo kwenye miili yao kuonyesha upendo walionao kwa wazazi ama wenzi wao. Wale wanaochora majina au kuonesha upendo kwa wazazi huwa hawapati shida baadae lakini wanaowachora wapenzi wao hupata shida ya kuzifuta pindi penzi linapokwisha.

Daktari

Hivi karibuni MTANZANIA limefanya mahojiano maalumu na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ngozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aneth Kissongo.

Anasema vijana wengi hupenda kujichora tattoo katika miili yao bila kujua kwamba zinaweza kuwasababishia madhara mbalimbali.

“Kwa kawaida, mtu anapochora ile tattoo mwilini mwake ile rangi huenda moja kwa moja hadi katika sehemu ya ndani ya ngozi iitwayo dermis,” anabainisha.

Anasema athari kubwa ambayo huweza kujitokeza wakati wa uchoraji wa tatoo ni watu kupata magonjwa ya maambukizi.

“Kile chombo kinachotumika ikiwa kimetumika kwa kundi kubwa la watu, kama wana magonjwa ya maambukizi kwa mfano Ukimwi, homa ya ini na mengineyo ni rahisi kuambukizana,” anasema.

Anasema wakati mwingine watu wanaweza kupata maambukizi ya bakteria (bacteria infection).

“Yaani wanaweza kupata vidonda ambavyo huwa haviponi haraka, kama umewahi kuona mtu aliyetoboa sikio halafu likawa halijapona vizuri basi wale wanaochora tattoo nao huweza kupata hali ya namna ile.

“Ile rangi inayotumika kuchora tattoo inaweza kumsababishia muhusika kupata mzio.

“Inapoingia mwilini hutengeneza kitu, kitaalamu tunaita contact dermatitis (mwili hupata vidonda vidonda, ni kama vile mtu aliyevaa saa akatoa au hereni akapata vidonda vidonda,” anafafanua. 

Watu weusi

Anasema athari huwa kubwa zaidi kwa Waafrika ambao kutokana na ngozi yao nyeusi huweza kupata makovu makubwa yasiyokuwa ya kawaida.

“Ngozi yetu Waafrika ni tofauti na ‘watu weupe’ wapo ambao baada ya kuchorwa na kupata tattoo walizohitaji hujikuta wakipata makovu makubwa yasiyo ya kawaida,” anasema.

Anatoa mfano: “Ni kama vile mtu aliyetoga sikio lakini badala ya kupata kitobo anachohitaji anajikuta nyama ikiendelea kushuka na kuongezeka, na tattoo hutokea hivyo hivyo.

Anasema wapo ambao makovu hayo hufika mahali na kuanza kupungua hata hivyo wengi huwa yanaongezeka ukubwa. 

Utafiti

Utafiti umebaini kuwa tattoo inaweza kumsababishia muhusika kupata saratani.

Hiram Castillo wa Kituo cha Radiation cha nchini Ufaransa ni miongoni mwa waandishi wa utafiti huo.

Wanasema kemikali za wino wa tattoo huweza kusafiri katika damu na kukusanyika katika mfumo wa lymph.

Hali hiyo huufanya mwili kuvimba na hivyo kuzuia uwezo wake wa kupambana na maambukizi dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Watafiti hao wanataja kemikali ya titan-dioksaidi ambayo hutumiwa kuunda wino mweupe ni miongoni mwa kemikali zinazoongeza hatari ya mtu kupata saratani.

“Mtu anapotaka kupata tattoo, mara nyingi huwa makini sana katika kuchagua sindano ambazo hazikutumika awali lakini hakuna mtu anayeangalia kemikali ya rangi, lakini utafiti wetu unaonesha wanapaswa kufanya hivyo,” anasema Castillo.

Wanasayansi hao wa Ufaransa na Ujerumani walitumia X-rays na kipimo cha fluorescence kuchunguza chembe ndogo, waliripoti ushahidi mkubwa unaoonesha kwamba wino wa tattoo huzunguka mwili kabla ya kujenga amana (depostis).

Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika majarida mbalimbali pamoja na mtandao wa daily mail Septemba 12, mwaka huu.

Je, inafutika?
Ni ngumu mno kuifuta tattoo na hii ni changamoto kwa watu waliochora majina au sura za wapenzi wao wa zamani. Kuna kikaa kinaitwa laser ambacho kinaweza kutumika kufuta tattoo yote au sehemu ndogo tu ya tattoo, mara nyingi rangi nyeusi zinaweza kutoka ukilinganisha na zingine. Maumivu anayoyapata mhusika ni makali kuliko maumivu ya kuiweka.

Dk. Aneth anasema mara nyingi katika kitengo chicho wamekuwa wakipokea vijana wengi wanaohitaji huduma ya kufutwa tattoo walizojichora mwilini.

“Wanapohitimu masomo wengi huja wakitaka kufutwa, ingawa siwezi kueleza idadi yao kwa sasa lakini mara nyingi huwa ni wale waliohitimu masomo yao na huwa wanahitaji kujiunga na fani mbalimbali,” anasema.

Anaongeza: “Wengi hujikuta wakikosa ajira kwa sababu michoro ya tattoo huwa haifutiki, kwa sasa hatuna uwezo wa kuzifuta.

“Unajua mtu akichora tattoo humfanya mtu mwingine kutafakari yeye ni mtu wa namna gani, lakini kuna taaluma fulani fulani ambazo mtu aliyechora tattoo hatakiwi kujiunga.

“Kwa sababu inakuwa ni sawa na amejiweka muhuri fulani na hivyo kuonekana hafai kwa kazi husika, zipo pia kazi zingine ambazo mtu mwenye kovu hawezi kupata nafasi kuifanya,” anasema.

Kuna kampuni mbalimbali duniani haziajiri watu waliochora tattoo kulingana na imani za zao, lakini pia kazi yoyote ya jeshi duniani hairuhusu tattoo. 

Nini kifanyike kwa wanaopenda?
Siku hizi kuna tattoo zinachorwa juu ya ngozi kama hina na kuondoka baada ya muda fulani, hizi hazina madhara kabisa. Huchorwa kwa bei ndogo na hukupa fursa ya kuzibadili pindi mhusika anapoichoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles