23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DAWA ZA KULEVYA ZINAVYOWEZA KUSABABISHA UTEJA


NA JACKSON NYABUSANI

DAWA za kulevya katika tafsiri ya kawaida tunasema ni kile kitu kinachotumika kutibu na kuzuia magonjwa yaliyopo katika jamii zetu.

Kulingana na aina ya dawa na namna ambavyo inatumika, kuna vitu ambavyo hujitokeza lakini vikubwa ni hivi viwili: Kwanza kuna mambo ambayo dawa huyafanya katika mwili na pili kuna mambo ambayo mwili huyafanya katika hiyo dawa mara baada ya kutumika.

Mada ya leo inayohusu dawa za kulevya tutajifunza mambo ambayo dawa hizi  hufanya katika mwili na kusababisha ziitwe dawa za kulevya.

Ili dawa iweze kuitwa kuwa ni ya kulevya huwa na sifa au tabia ya kuufanya mwili au mtumiaji ashindwe kujitawala katika kuzitumia, katika hili mtumiaji ataitumia dawa bila ya kipimo, bila ratiba, bila tahadhari yoyote ilimradi tu mwili wake uwe umeipata dawa hiyo.

Pili ni mtumiaji pindi akiacha kuzitumia anapata dalili mbaya kimwili au kiakili na hivyo kumfanya azitafute dawa hizo ili atumie kwa dhumuni la kuondokana na hali mbaya anayoihisi mwilini mwake.

Sifa hizo humfanya mtumiaji awe mteja wa dawa hizo kwa maana ya kuhitaji mara kwa mara wa dawa. Hali hii kwa jina la kitaalamu huitwa ‘Drug Addiction’ au kwa Kiswahili ‘Uteja au Teja.’

Yapo mambo yanayomfanya mtu aanze kutumia dawa za kulevya hadi kufikia hatua ya kuwa teja, miongoni mwa mambo hayo ni kuwa na marafiki wanaotumia dawa hizo na hivyo ili kuendeleza urafiki anajikuta anaanza kutumia ili asiwaangushe marafiki zake (mob psychology).

Urafiki unaweza kuwa ni katika mazingira ya shule, shughuli za michezo na sanaa na maeneo mengine.

Msongo wa mawazo; mtu anaona akitumia dawa hizi itamsaidia kuondoa mawazo yaliyomjaa kichwani ambayo hayampatii furaha yoyote katika maisha yake.

Mtu kutaka kujaribu kutumia kila kitu, hii inatokea kwamba mtu hana sababu zozote zile ila tu anataka ajaribu kutumia dawa hizo ili aone nini kitatokea mwishowe anakuwa teja.

Inawezekana ungependa kufahamu ni kwa nini dawa hizi husababisha mtu awe teja wakati kuna dawa nyingi ambazo hazisababishi hali hii.

Utendaji kazi wa dawa hizi mwilini tunazoziita za kulevya ni mgumu, ila kuna sifa mbili zinazoweza kulielezea jambo hili.

Kwanza inahusika na mwili wa binadamu hususani sehemu kuu ambapo dawa hizi za kulevya huhusika kama katika mfumo wa fahamu (ubongo).

Ubongo wa binadamu umeumbwa kwa chembe hai (Cells) ambazo ni laini mno (Very Delicate) ukilinganisha na seli za sehemu nyingine ya mwili, hivyo ni rahisi kubadilika kutegemeana na mazingira unayouzoesha ubongo wako, jinsi utakavyo uzoesha ndivyo utakavyo kuwa.

Pili ni sifa ya dawa zenyewe za kulevya, ambapo zina sifa ya kubadilisha utendaji kazi wa chembe hai (Cells) katika mfumo wa fahamu na kuzifanya zifanye kazi kuendana na dawa yenyewe husika, hivyo ubongo wako hautojitawala bali kazi za ubongo zitatawaliwa na dawa, kwa kuwa seli za ubongo ni rahisi kubadilika, itasababisha utendaji kazi wake utazoea (adaptation) kufanya kazi kwa msaada wa dawa na hivyo ukiacha kutumia unajikuta mwili/ubongo hauko tayari kufanya kazi bila dawa hatimaye utaanza kuitafuta ili ubongo uweze kurudi katika hali iliyozoea ya kutumia dawa na hii ndiyo huitwa uteja/teja.

Uteja unayo madhara kwa teja mwenyewe na hata kwa jamii na taifa kwa ujumla, mtu unapokuwa teja kwanza unaudhalilisha utu wako, unashindwa kushiriki kikamilifu katika mambo ya kijamii/kazi, unakuwa katika hatari (risk) ya kupata magonjwa mbalimbali kutokana na kuchangia vitu vyenye ncha kali (sindano, viwembe) na pia huchangia familia nyingi ziwe na migogoro.

Kila mwanajamii analo jukumu la kumuelimisha mwenzake juu ya athari zinazotokana na utumiaji wa dawa zinazosababisha mtu kuwa teja na kwa wale ambao kwa bahati mbaya wamepata tatizo hili, uwezekano wa kupona upo. Jambo la kufanya ni kuonana na wataalamu wa afya ili kupata msaada  stahiki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles