WASHINGTON-MAREKANI
WAKAGUZI wa Marekani wamegundua tatizo jipya katika ndege ya kampuni ya Boeing chapa 737 max ambalo huenda likachelewesha kwa ndege hiyo kurudi.
Hayo yamebainika baada ya ajali mbili kubwa ya ndege ya Ethiopia ET302 yenye chapa ya 737 Max, Machi mwaka huu na ile inayokaribiana kufanana na hiyo inayomilikiwa na kampuni ya Indonesia Lion Air, iliyoanguka baharini Oktoba 2018.
Utawala wa safari za anga nchini Marekani-Federal Aviation Administration (FAA) umesema wakati wa majaribio wamegundua “kinachoweza kuwa ni hatari “.
Hata hivyo FAA haukuweka wazi matokeo ya hicho kinachotajwa kuwa ni hatari.
Ndege hiyo inayouzwa sana katika kampuni ya Boeing ilisitishwa Machi baada ya ajali hizo mbili kubwa.
Kabla ya taarifa za sasa ripoti za awali katika ajali zote ziliashiria kusababishwa na matatizo katika mfumo wa ndege kutua uliochelewa kufanya kazi kwa muda muafaka kutokana na hitilafu katika sensa yake.
Kampuni hiyo inamarisha mfumo wa kutua kwa ndege hiyo, ambao unachunguzwa na maafisa wa uchunguzi wa ajali ya ndege.
Katika ujumbe wao kwenye twitter, FAA wamesema wamebaini hatari zinazowezekana kuwepo ambayo ni lazima Boeing itatue.
Mwezi uliopita, FAA waliashiria kuridhia mabadiliko ya Boeing kwa ndege hiyo ya 737 Max ambayo yanaweza kuidhinishwa mwishoni mwa Juni.
Hatua hiyo ingeruhusu ndege hizo kufanyiwa majaribio mapema mwezi Julai.
Awali kulikuwa na matumaini kuwa ndege ya 737 Max itarudi angani wakati wamsimu wa joto, lakini hilo huenda likawa tofauti hasa baada ya taarifa hizi mpya.
Reuters, ambao walikuwa wa kwanza kuripoti tatizo hilo limesema kuwa wakati wa kufanyiwa majaribio kwenye usukani wa rubani ambako kuna mfumo wa kutua, ilichukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa kupata udhibiti wa ndege hiyo.
Vyanzo vingine vinasema tatizo linahusiana na nguvu ya kompyuta ya ndege hiyo na huenda haukuwa na uwezo wa kupokea maagizo kwa kasi inayohitajika.
Boeing imesema “Tunashirikiana kwa karibu na FAA kuirudisha huduma ya ndege ya Max “.
Imesema inaamini suluhu katika mfumo huo utalitatua tatizo lililopo.
Inaelezwa iwapo wakaguzi hawatapata suluhu, mfumo itabidi ubadilishwe na huenda ikachukua muda wa ndege hiyo kurudi.
BBC