Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
NI pigo ndani ya tasnia ya habari. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mpiga picha mahiri na mwanahabari mkongwe, Mpoki Bukuku (44), kufariki dunia jana.
Mwanatasnia huyo wa habari alikumbwa na umauti saa 11.06 alfajiri wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI).
Marehemu Bukuku alifikishwa juzi usiku katika Taasisi ya MOI akitokea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako alipelekwa kwa matibabu baada ya kupata ajali mbaya ya kugongwa na gari kwenye kituo cha daladala cha ITV kilichopo Mwenge, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Taarifa ambazo gazeti hili limeambiwa zinadai kuwa marehemu Bukuku aligongwa na gari wakati akivuka Barabara ya Bagamoyo, akitokea ofisi za Kampuni ya The Guardian alikokuwa anafanyia kazi.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa MOI, Almas Jumaa, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.
“Ni kweli, Mpoki amefariki dunia leo (jana) saa 11.06 alfajiri wakati madaktari wakiendelea kumsaidia kuokoa maisha yake… tulimpokea MOI saa nne usiku kutoka MNH, taarifa iliyoandikwa na daktari inaeleza kuwa alikuwa amevunjika mbavu tatu za upande wa kushoto wa mwili wake, mkono wa kushoto na miguu yake yote miwili ilikuwa imevunja,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa ripoti hiyo, alikuwa ameumia upande wa kushoto wa mwili wake inahisiwa kwamba huenda gari lilimgonga upande huo au aliangukia upande huo wa kushoto, pia alikuwa akilalamika kupata maumivu ya ndani (internal pain) hivyo ikabidi wamuwekee ‘tube’ ya kutolea uchafu ubavuni.
“Inasikitisha mno, tasnia imepoteza mtu makini, imepoteza kigogo,” alisema.
Katika taarifa yake aliyoituma kwa vyombo vya habari jana Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya The Guardian, Richard Mgamba, alisema tasnia ya habari imepoteza nguzo muhimu.
“Leo (jana), kama ilivyo kwa wengine wengi, nimepokea kwa mshtuko mkubwa na kutoamini, kuhusiana na kifo cha ghafla cha mmoja wa wapigapicha waandamizi wa The Guardian Limited, Bw. Mpoki Bukuku (44), aliyefariki asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Kwa familia yake, wamempoteza baba, mume na zaidi ya yote rafiki wa kweli, lakini kwetu sisi The Guardian Limited, tumempoteza pia rafiki wa kweli na nguzo katika tasnia ya uandishi wa habari,” alisema.
Aliongeza: “Bukuku alikuwa ni mwanadamu tu kama ilivyo kwa yeyote kati yetu, lakini katika uandishi wa habari, alikuwa ni mtu aliyeipenda fani yake na hakuogopa kupambana alimradi apate habari nzuri. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana kuna wakati kiu yake ya kupata habari nzuri kuliko wengine wote ilimuweka matatani.
“Wale wanaoelewa uandishi wa habari wa picha watabaini kwamba ujasiri na kuipenda kazi ni sifa kuu mbili za kila mpigapicha ili kupata habari nzuri na yenye nguvu. Bukuku alikuwa na sifa zote hizo mbili. Alikuwa shujaa na mwenye mapenzi na kazi yake hasa wakati akifuatilia habari kubwa kokote kule katika nchi hii.
“Alipigwa na hata kuteswa na maadui wa uhuru wa vyombo vya habari, lakini bado mahaba yake katika kufanikisha habari bora hayakuzimwa. Alikuwa ni mwandishi wa habari si kwa bahati mbaya, bali ni kwa kuchagua na ndiyo maana alikuwa na mapenzi wakati akitimiza wajibu wake wa kutekeleza kazi mbalimbali za kihabari alizopangiwa na wahariri wake,” alisema.
Alisema Bukuku amemaliza safari yake duniani, kimwili hayuko nasi lakini kiroho na kiuweledi, mara zote atakuwa nasi daima.
“Sisi katika Kampuni ya The Guardian Limited, tunaungana na familia, ndugu na marafiki katika kipindi hiki kigumu, kuomboleza msiba wa mtu ambaye tumekuwa tukifanya naye kazi kwa miaka mingi. Kampuni itaiunga mkono kwa ukamilifu familia ya marehemu Bukuku.
“Kwa niaba ya wafanyakazi wote wa The Guardian Limited, kwa heshima kubwa natoa salamu zangu za rambirambi kwa mjane wa Bukuku, Lucy, watoto na wadau wote wa tasnia ya habari nchini Tanzania, kwa kifo cha ghafla na kushtua cha mmoja wetu,” alisema.
Naye Grace Nacksso ‘Graphic Designer’ wa magazeti hayo ambaye alikuwa naye zamu siku hiyo katika ‘group’ moja la whatsup aliandika: “Imeniumiza sana. Jana usiku tumefanya kazi vyema na alikuwa mpole tofauti kabisa na siku zote. Hadi mimi ndiye niliyekuwa namchokoza.
Aliendelea: “Uwepo wa Mpoki newsroom ikiwa ni zamu yake, watu wengi wanaujua. Lazima kuwe na tukelele fulani twa hapa na pale na vicheko vingi. Ni vijimambo tu vya kazini. Tunapigiana kelele za hapa na pale nikimtaka anikabidhi picha tumalize kurasa.
Aliendelea: “Lakini kwa jana haikuwa hivyo. Alipooza sana mpendwa yule. Ni ngumu kuamini kuwa alikuwa anaenda kufa. Sasa ndio ninaamini kuwa hakuna aijuaye kesho yake.”
“Tangulia mpambanaji Mpoki, laiti sisi wenzako tungejua kuwa pale ulituaga kuwa unakwenda kupoteza maisha, Mungu angetuongoza tungekuchelewesha chelewesha kidogo kama inavyokuwa siku zote hivyo ungeondoka na staff wote na hayo yasingekupata.
Lowassa atoa pole
Mjumbe wa Halmashauri Kuu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, alitoa salama za pole kwa wote walioguswa na msiba huo.
“Nimesikia taarifa za kifo cha mpigapicha mahiri, Mpoki Bukuku, nimesikitika mno, natoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wote waliofikwa na msiba huu,” alisema jana katika mkutano wake na wanahabari.
CUF
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi Taifa (CUF), Julius Mtatiro, katika ukurasa wake wa facebook aliandika: “Nimeumizwa sana na kifo cha mpigapicha wa gazeti la The Guardian, Mpoki Bukuku… kwanini hukutuaga jamani? Poleni sana The Guardian!! RIP Mpoki! Tangulia brother, tuko nyuma yako. Poleni ndugu na marafiki wote.
Historia yake
Bukuku amewahi kufanya kazi kama mpiga picha mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanasporti.
Pia amewahi kufanya kazi na kampuni nyingine ikiwamo Business Times Ltd wachapishaji wa gazeti la Majira.
Aidha, alikuwa akipasha habari kupitia blog zake mbili maarufu kama mzee wa sumo na saahiihii.
Uongozi wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd unatoa pole kwa wote walioguswa na msiba huu hasa familia ya marehemu.
Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.