27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI YAPIGA MARUFUKU DISKO TOTO

disko-toto

Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limepiga marufuku kufanyika kwa burudani za watoto maarufu kama disko toto katika kumbi mbalimbali za starehe wakati wa Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya wa 2017.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Operesheni Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi, Lucas Mkondya, alisema hatua hiyo imefikiwa kutokana na madhara yaliyowahi kutokea siku za nyuma.

“Tunapenda kutoa tahadhari katika maeneo ya fukwe watoto kuzagaa bila ya uangalizi wa wazazi au walezi wao. Polisi watakuwa doria maeneo mbalimbali ili kuhakikisha vitendo vyote vinavyoweza kuleta madhara au kutokea kwa uhalifu vinazuiliwa mapema,” alisema Mkondya.

Pia alisema Jeshi hilo limejipanga kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa kutosha katika kipindi chote hiki ili wananchi washerehekee sikukuu kwa amani na utulivu kutokana na vitendo vingi vya uhalifu vinavyofanywa na watu wenye nia ovu.

Alisema polisi itaimarisha doria katika maeneo mbalimbali ya jiji ikiwa ni pamoja na kupeleka askari katika kila kanisa ili kuhakikisha ibada zinafanyika katika hali ya amani.

“Tutatumia askari wenye sare na makachero watakaofanya ulinzi maeneo mbalimbali, lakini pia tutatumia helikopta kuimarisha ulinzi zaidi na tutahakikisha kila mtaa unakuwa na askari wakishirikiana na mgambo au walinzi shirikishi.

“Wananchi wanatakiwa kuwa waangalifu kwa kutokunywa vileo kupita kiasi, kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuzua ugomvi na mambo mengine kama hayo,” alisema Mkondya.

Aliwataka wananchi watakaokwenda katika fukwe za bahari kuwa waangalifu na wachukue tahadhari kwa kutowaruhusu watoto kuogelea peke yao na kuepuka kuogelea wakiwa wametumia vileo jambo linaloweza kusababisha madhara.

Pia aliwataka watakaotumia magari binafsi kuhakikisha wanayaegesha katika maeneo salama na kuyafunga vizuri huku akiwataka wananchi kutoa taarifa sehemu husika pale wanapoona viashiria vya uhalifu ili wapate msaada.

Katika hatua nyingine, wamefanikiwa kukamata gari aina ya Toyota Spacio lenye namba za usajili T 398 CAE, televisheni moja aina ya Samsung na sanduku la kuhifadhi fedha ingawaje kiasi cha fedha kilichokuwamo hakijajulikana hadi sasa vyote vikiwa ni mali ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA).

Alisema Desemba 5, mwaka huu walipokea taarifa za kuvunjwa kwa ofisi za TIRA zilizopo Kisutu, Dar es Salaam kutoka kwa Msimamizi Mkuu wa TIRA, Egnace Edward na wakaanza kufanya msako wa kuwabaini waliohusika katika tukio hilo.

“Watuhumiwa wanne wamekamatwa kama ifuatavyo; Leonard Said, Omary Said, Shomaly Kilobo na Adam Unemba, watuhumiwa wote walikiri kuhusika katika tukio hilo la uvunjaji,” alisema Mkondya.

Alisema watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili pindi upelelezi utakapokamilika.

Katika tukio jingine, watu 176 wametiwa mbaroni kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya unyang’ayi wa kutumia nguvu, kuvunja nyumba usiku na kuiba, wizi wa magari na mengineyo.

“Operesheni iliyofanyika Kimara na Mbagala jumla ya watuhumiwa 76 walikamatwa kwa makosa mbalimbali na jumla ya lita 359 za pombe haramu ya gongo zilikamatwa, mitambo ya kutengenezea gongo na bangi, pia watuhumiwa hao walikutwa na silaha ndogo ndogo za kufanyia uhalifu kama vile visu, nyembe na bisibisi,” alisema Mkondya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles