25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

TASAF YAFANIKIWA KUONDOA UMASIKINI

Na FARAJA MASINDE-ALIYEKUWA PWANI

TANZANIA ni miongoni mwa nchi barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa haraka kwa wastani wa asilimia 7 ikilinganishwa na nchi nyingine.

Licha ya kwamba kumekuwapo na changamoto mbalimbali katika kustawi kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja, bado kama nchi imebakia kwenye orodha ya mataifa yanayostawi kwa haraka  kiuchumi.

Tatizo kubwa la nchi kiuchumi ni umasikini ambao haulingani na ukuaji wa uchumi kwa miaka ya hivi karibuni  na hivyo kushuhudia jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali kwa nyakati tofauti katika kuhakikisha kwamba uchumi wa wananchi hususan wa hali ya chini unaimarika.

Umasikini  unaelezwa kuwa ni kushindwa kujimudu kwa mahitaji muhimu ya kawaida kwa maisha ya mtu na jamii ikiwamo kipato, rasilimali na ujasiriamali.

Kwa vipindi tofauti, Serikali kupitia mifuko na taasisi zake mbalimbali imeendelea kuwa nguzo ya uchumi wa wananchi kupitia kutoa mitaji, elimu, kutoa mafunzo mbalimbali ya namna ya kujihusisha na shughuli za kiuchumi ili kujiletea maendeleo na kupunguza umasikini.

Itakumbukwa kuwa awali Serikali ilianzisha Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (Mkukuta), ukiwa ni mpango wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia inayozingatia matokeo ili kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na kukabiliana na changamoto za kukuza uchumi na kupambana na umasikini nchini.

Taarifa zinaonyesha kuwa kupitia mpango huo, bado kiwango cha umasikini wa kipato kwa wananchi hakijaweza kuleta matokeo chanya, katika Watanzania 100, ni Watanzania 36 walikuwa na umasikini wa kipato kwa mwaka 2000 ambapo hadi kufikia 2007  Watanzania 34 bado walikuwa wanakabiliwa na umasikini.

Kufuatia kushindwa kuleta matokeo chanya kwa mpango huo, Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, iliamua kuja na mpango mpya, lengo likiwa ni moja tu la kuhakikisha kuwa inawakwamua Watanzania wanaokabiliwa na mazingira magumu kwa maana ya kaya masikini.

Hivyo Serikali iliamua kuwekeza nguvu kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), lengo likiwa ni katika kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.

Kwa kawaida Tasaf imekuwa ikisimamiwa pamoja na kutengewa fedha na Serikali, ikiwamo pia kupata ufadhili kutoka kwa wadau wa maendeleo ambao ni Benki ya Dunia (WB), Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Serikali ya Marekani (USAID) na Serikali ya Uhispania (Spain).

Mfuko huu umekuwa ni mkombozi mkubwa katika kusaidia wananchi kuondokana na umasikini ambapo jitihada mbalimbali za kuwawezesha kiuchumi zimefanyika kuanzia awamu ya kwanza hadi sasa awamu ya tatu.

Hayo yanadhihirishwa na jitihada za Tasaf  ambapo hadi kufikia kaya milioni 11, nchi nzima zimenufaika na mpango huu huku Sh bilioni 431 zikitumika kulipa wanufaika wa mpango huo kote nchini.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga, anasema  mpango huo umekuwa na manufaa makubwa katika kuinua uchumi wa Watanzania, huku akiutolea mfano Mkoa wa Pwani ambao wananchi wake wamefanikiwa kujikwamua na umasikini kwa kiwango kikubwa chini ya Tasaf.

Anasema mradi wa uhawilishaji fedha ni mradi unaolenga kutoa ruzuku kwa kaya lengwa ili kuziwezesha  kumudu gharama za maisha kwa kuziwezesha kupata mahitaji ya msingi. Na kwamba mradi huo una aina kuu mbili za ruzuku ambazo ni ya msingi na ile ya masharti.

Kwa Mkoa wa Pwani, Mpango huu ulianza Januari mwaka 2014 katika halmashauri za wilaya za Bagamoyo na Kibaha kwa majaribio. Kwa kipindi cha Januari mwaka 2014 hadi Januari mwaka  2017, wilaya zilifanya malipo kwa mizunguko 19 ambapo kiasi cha Sh bilioni 11.11  zilitengwa, Bagamoyo ikipata bilioni 8.09 huku Kibaha ikipata bilioni 3.021 zilizotolewa kwa walengwa 15,920.

Baadaye mpango ulipanuka na kuenea katika halmashauri za wilaya za Mkuranga, Kibaha Mjini na Mafia. Wilaya hizo  zilianza kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mwezi Julai, 2015 ambapo hadi Desemba, 2016 zilikuwa zimeshalipa mizunguko 10.

“Mwaka 2015, tulianza kutekeleza miradi ya kutoa ajira za muda kwa walengwa, miradi hii inaziwezesha kaya lengwa zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoibuliwa na jamii husika na kulipwa ujira.

“Awali mpango huu ulianza kutekelezwa katika halmashauri mbili za Bagamoyo na Kibaha, kwa mwaka wa fedha 2015/ 2016, Mkoa ulitengewa Sh bilioni 2.1 kwa miradi 192 iliyotekelezwa katika vijiji 111 vilivyopo katika halmashauri ya wilaya za Bagamoyo (66) na Kibaha (45), miradi hiyo ni ukarabati wa barabara za vijijini, ukarabati wa mabwawa, upandaji wa vitalu vya miti aina ya mikoko ambayo imekuwa na faida kubwa kwa wananchi pindi inapokomaa,” anasema Mwamanga.

Anabainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017, jumla ya miradi 156 inatekelezwa katika wilaya tatu kati ya saba (Bagamoyo 68, Kibaha 45 na Kisarawe 43) kupitia miradi hiyo, Mkoa wa Pwani umepokea kiasi cha Sh bilioni 504.2 ambapo Sh bilioni 63.3 zikiwa ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo wananchi na kiasi cha Sh bilioni  440.8, ikiwa ni kwa ajili ya kununua vitendea kazi ambapo miradi hiyo imeibuliwa katika wilaya za Bagamoyo, Kisarawe na Kibaha na utekelezaji wake upo katika hatua za awali.

“Miradi hii inalenga katika kujenga uwezo kwa walengwa ili waweze kuweka akiba kidogokidogo wakiwa katika vikundi na kukopeshana. Lengo likiwa ni kuongeza kipato kwa kaya masikini kupitia uwekaji wa akiba na shughuli za kiuchumi ili kuboresha maisha.

“Kupitia miradi ya uhawilishaji fedha na ajira za muda, kaya masikini zimeanza kuwa na uhakika wa kujikimu katika maisha yao ya kila siku na kuanza kuweka akiba. Kutokana na kutolewa kwa ruzuku ya masharti ya elimu, watoto kutoka kaya masikini wameweza kuhudhuria shule vizuri na hivyo kuongeza ushiriki wao katika masomo,” anasema Mwamanga.

Anabainisha kuwa lengo kuu la mfuko huu ni kuziwezesha jamii zenye kipato cha chini kuinua hali zao za kimaisha kwa kuanzisha shughuli zitakazoinua uchumi wao kupitia taasisi kuanzia ngazi ya kikundi na hatimaye vikundi vitaunda jumuiya na hata kuunda shirikisho la kuwakomboa.

“Serikali imeendelea na jitihada za kupunguza umasikini kwa kusimamia utekelezaji wa Awamu ya II na III ya Tasaf, kwa lengo la kuhamasisha jamii yenye kipato cha chini kujiwekea akiba na kuwekeza, lengo likiwa ni kila Mtanzania kuweza kuondokana na umasikini,” anasema.

Upande wa Benki Kuu ya Dunia ambao ndio wamekuwa wafadhili wakubwa wa fedha za mradi huu kwa kushirikiana na Serikali, inaweka wazi namna ambavyo imeweza kuvutiwa na namna fedha hizi zinavyotumika.

Kiongozi wa WB anayeshughulikia miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), Mohammed Mderis, anasema Tanzania ni moja ya nchi barani Afrika ambayo inatumia vizuri fedha za miradi inayofadhiliwa na benki hiyo kwa kushirikiana na Serikali.

“Ni jambo la faraja kuona fedha zinazotolewa nchini Tanzania  na Benki ya Dunia zinatumika vizuri na zimeleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi.

“Ukitazama kwa Afrika, Tanzania imekuwa ni namba moja kwa kutumia vizuri fedha hizi, jambo hili limetupa moyo,” anasema  Mderis.

Heleh Bridi ambaye ni Mkurugenzi wa Uhusiano wa Nje wa WB, anasema   kulingana na miradi aliyotembelea na ushuhuda mbalimbali alioupata  kutoka kwa wananchi wa kaya zinazonufaika, ni wazi fedha wanazozitoa ziko kwenye mikono salama.

“Jitihada hizi zinazofanywa na Tasaf kwa  kushirikiana kwa ukaribu kabisa na Serikali, ni wazi kuwa zinatupa hamasa ya kuendelea kushirikiana na Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles