Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
WAKALA wa Barabara Vijijini (TARURA) Wilaya ya Ilala, imekamilisha ujenzi wa daraja la Mto Mzinga, Kata ya Kivule juzi ambalo lilichukuliwa na mvua na kusababisha wananchi kukosa mawasiliano kwa miezi mitatu.
Daraja hilo jipya limezinduliwa juzi na kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Charles Kebeho ambaye alisifu ujenzi huo ambao aliuita wa kiwango bora.
Mmoja wa wakazi wa kata hiyo, Ester Samson, alisema daraja hilo ni mkombozi kwao kutokana na adha kubwa waliyokuwa wakiipata awali.
“Daraja hili limetutesa sana sisi kina mama wa kata hii, ambao ndio tunapeleka watoto kliniki pamoja na wazee kupata matibabu ng’ambo ya pili,” alisema mkazi huyo.
Naye Kebeho akizungumza wakati wa uzinduzi huo, alisifu kazi nzuri iliyofanywa na uongozi wa Tarura Wilaya ya Ilala na kuwataka waendelee kutekeleza miradi katika viwango ambavyo vimeonekana katika daraja hilo.
“Nawapongeza sana Tarura kwa kazi nzuri mliyoifanya hapa, fanyeni na maeneo mengine, hii ni moja ya kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wetu, John Magufuli,” alisisitiza.
Meneja wa Tarura Wilaya ya Ilala, Samweli Ndoveni, alisema daraja hilo limetengenezwa kwa muda mfupi, lakini wamejiridhisha kwamba lipo katika ubora unaotakiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, alisema Serikali itaendelea kutatua kero za wananchi kwakuwa inawajali na kuhakikisha wananchi wote ndani ya wilaya yake wanapata mahitaji yao, hususani kutatuliwa kero ya miundombinu ya barabara.
Diwani wa Kata ya Kivule, Willison Molleli, aliwapongeza Tarura Ilala kwa kazi ya kukamilisha daraja hilo lililokuwa kikwazo kwa wananchi.