23.5 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

TARURA yafanya matengenezo ya barabara wilayani Maswa

Na Samwel Mwanga, Maswa

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu  umeendelea kuzifanyia matengenezo barabara zake katika wilaya hiyo katika maeneo mbalimbali ili kuwezesha wananchi kufika sehemu ambazo awali zilikuwa hazifikiki.

Meneja wa Tarura wilaya ya Maswa, Mhandisi David Msechu amesema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea barabara ya Bugarama-Mwabomba hadi Mwanundi inayofanyiwa matengenezo kwa kiwango cha Changarawe kwa gharama ya Sh milioni 500.

Amesema wilaya hiyo yenye mtandao wa barabara zenye urefu wa Kilomita 1804.4 zimekuwa zikifanyiwa marekebisho ya mara kwa mara hasa kwenye maeneo korofi ambayo hayawezi kupitika kwa kipindi chote cha mwaka hasa nyakati za mvua.

Mhandisi Msechu amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu kwani itasaidia wananchi kutoa mazao yao mashambani na kusafiri kwa urahisi kutoka katika maeneo hayo kupeleka mjini Maswa na wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

’’Barabara hii itakapokamilika itarahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi maana kuna shughuli za kilimo zinafanyika katika maeneo haya hivyo wataweza kwenda kuuza mazao yao mjini Maswa na wilaya jirani ya Kishapu iliyoko mkoa wa Shinyanga,” amesema Mhandisi Msechu.

Pia amesema wananchi wengi walikuwa wanashindwa kufika kwa wakati wanapohitaji huduma ya Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa na Kituo cha afya cha Mwasayi hivyo kukamilika kwa barabara hiyo kutaondoa adha hiyo.

Aidha, Meneja huyo amefafanya kuwa fedha itakayotumika kujenga barabara hiyo imetolewa na Serikali ikiwa ni sehemu ya Sh bilioni moja iliyotolewa kila jimbo la uchaguzi ambapo Maswa Magharibi zimetumika kutengeneza barabara hiyo.

Amesema kampuni ya Ujenzi ya RIHA Construction Company Ltd ya jijini Mwanza ndiyo imepewa kazi ya kufanya matengenezo hayo kwa mkataba wa miezi sita kuanzia Novemba 22, 2021 hadi Mei 21, mwaka huu na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 80.

Naye Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa kwa sasa serikali inapeleka fedha nyingi TARURA  kwa lengo la kuhakikisha maeneo yenye changamoto katika barabara yanafanyiwa kazi ili kuhakikisha wananchi wanazifikia huduma za kijamii kwa urahisi.

Baadhi ya wananchi ukarabati wa barabara hiyo wamesema kuwa imekuwa haipitiki kwa muda mrefu hivyo wamekuwa wakipata wakati mgumu pindi wanapohitaji huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa na kituo cha afya cha Mwasayi sambamba na shughuli zao za kiuchumi za kusafirisha mazao na kupeleka kwenye masoko.

“Hii barabara imekuwa mbovu kwa muda mrefu sana tumekuwa tukipata wakati mgumu kwenda kupata huduma za afya mjini Maswa na kwenye kituo cha afya cha Mwasayi pia huku sisi ni wakulima wa mazao ya chakula na biashara hivyo tulikuwa tunashindwa kuyafikisha mazao yetu kwenye masoko na ukizingatia kuwa tuko jirani ya wilaya ya Kishapu ya mkoa wa Shinyanga ambapo kwenye mji wa Mhunze kuna mnada mkubwa sana wa kuuza bidhaa mbalimbali yakiwemo mazao tunayozalisha,” amesema Hamad Khija mkazi wa kijiji cha Bugarama.

Wamesema kuwa kwa kitendo cha serikali kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara ni jambo jema hivyo wamemuomba Rais Samia Suluhu kuendelea kutoa fedha kwa TARURA ili waweze kuendelea kufungua barabara na kuzifanyia matengenezo zile mbovu ili ziweze kupitika kwa kipindi chote na wananchi wafikiwe na huduma kwa urahisi hasa katika maeneo ya vijijini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles