25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

TARI yawapa mbinu mpya wakulima kupambana na viwavijeshi

Na Derick Milton, Simiyu

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imewapa wakulima mbinu mpya ya upulizaji wa dawa kwa ajili ya kuua wadudu aina ya viwavijeshi (funza) ambao wamekuwa wakishambulia mahindi kwa kiwango kikubwa.

Taasisi hiyo imesema kuwa wakulima wengi, wamekuwa wakipuliza dawa nyakati za mchana au asubuhi kuua wadudu hao, muda ambao umeelezwa kuwa siyo rafiki funza hao kufa.

Mratibu wa usambazaji Teknologia za kilimo kutoka taasisi hiyo Mshaghuley Ishika, amesema kuwa mbinu mpya ambayo TARI wamekuja nayo ni kuwataka wakulima kupuliza dawa ya kuua wadudu hao nyakati za usiku.

Ishika amezungumza hayo Februari 9, mbele ya wakulima, maafisa ugani, kutoka katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara wakati wa maazimisho ya siku ya mkulima shambani, yaliyofanyika katika kituo cha usambazaji teknologia za kilimo Nyakabindi kilichopo halmashauri ya mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.

Mratibu huyo amesema kuwa TARI imegundua kuwa dawa ya kuua wadudu hao ikipuliziwa nyakati za mchama siyo rahisi kuwaua, kwani muda huo wanakuwa wameinamisha vichwa chini na miguu juu.

“Ukipuliza wakati vichwa vyao viko chini siyo rahisi kufa, inatakiwa vichwa vyao viwe juu, lakini mchana vinakuwa chini na miguu inakuwa juu, hivyo wakulima mnashauliwa kupuliza nyakati za usiku,” amesema Ishika.

Amesema kuwa taasisi hiyo inawashauri wakulima kutumia mbinu mpya ya upuliziaji dawa, ambapo amewataka kupulizia usiku muda ambao wadudu hao vichwa vyao vinakuwa juu na ni rahisi kufa.

“Tunawashauri wakulima kupuliza nyakati za usiku ambapo funza wanakuwa wametoa vichwa vyao juu, kuliko mchana vichwa vinakuwa chini, hapo ndipo tutaweza kupamba na wadudu hao ambao wamekuwa wakiharibu mahindi,” amesema Ishika.

Katika hatua nyingine Ishika amewataka wakulima wa mikoa hiyo, kutumia kituo cha Nyakabindi kuhakikisha wanaongeza tija kwenye kilimo chao, ikiwemo kupata mafunzo ya kanuni bora za kilimo, pamoja na kupata mbegu bora.

Kwa upande wake Afisa Idara ya mafunzo huduma za Ugani na Utafiti kutoka Wizara ya Kilimo, Paschalina Hayuna, alisema kuwa Wizara imejipanga kuhakikisha kituo cha TARI Nyakabindi kinatoa huduma bora kwa wakulima.

Amesema katika kuhakikisha hilo, Wizara imeagiza taasisi ya kudhibiti ubora wa mbegu Tanzania (ASA) kuhakikisha wanasambaza mbegi nyingi kwa wakulima, ikiwa pamoja na kufungua duka la mbegu bora katika kituo hicho ili wakulima waweze kuzipata kwa haraka.

Akihitimisha maadhimisho hayo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Wilaya ya Itilima Benson Kilangi, ameiomba Wizara ya kilimo kuongeza kasi ya usambazaji wa mbegu bora kwa wakulima kwani mbegu ambazo zinauzwa kwenye maduka ya watu binafsi nyingi hazina ubora.

Aidha, Kilangi amepongeza kituo cha Nyakabindi kwa teknologia nyingi ambazo zimeanza kupatikana katika eneo hilo, huku akiwataka wakulima wa mikoa hiyo kutumia fursa ya uwepo wa kituo hicho kuzalisha kwa tija.

Nao wakulima walioshiriki maazimisho hayo yamepongeza uwepo wa kituo hicho, hasa katika upatikanaji wa mbegu bora za viazi lishe, ambazo wamekuwa wakiangaika kwa muda mrefu katika kuzipata.
Hata hivyo katika maazimisho hayo Mkuu huyo wa wilaya alifanya uzinduzi rasmi wa kituo hicho, ikiwa pamoja na kugawa mbegu mbalimbali kwa wakulima ambazo ni bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles